
Bi. Asha Abinallah Mkurugenzi kutoka Tech and Media Convergence (TMC)
Na Bora Mustafa,Arusha.
maipacarusha20@gmail.com
Katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2026, wadau wa sekta ya habari wamekutana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya tasnia hiyo, hususan katika kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Akizingumza Leo Aprili 29,2026 Mwenyekiti wa mkutano huo, Bi. Asha Abinallah Mkurugenzi kutoka Tech and Media Convergence (TMC), amesema kuwa mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, wataalam wa sekta hiyo pamoja na wasimamizi wa vyombo vya habari. Amesema washiriki wamejadili kwa kina masuala ya uzalishaji wa habari pamoja na usambazaji wake katika mazingira ya kidigitali.
![]() |
Aidha, amesema kuwa mjadala huo umeangazia namna vyombo vya habari vinavyoweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia, pamoja na kujadili nafasi ya teknolojia ya akili bandia (AI) katika sekta ya habari. Amesema AI inaweza kuwa fursa kubwa, hata hivyo inaweza pia kuwa changamoto endapo haitatumika kwa uelewa sahihi.
Pia amesema mkutano huo umehusisha zaidi ya mashirika ishirini kutoka Tanzania, pamoja na kukusanya maoni mbalimbali yatakayowasilishwa kwa serikali ili kusaidia kuboresha sekta hiyo. Aidha, amesema kuna umuhimu wa serikali kuanzisha mfuko maalum wa kusaidia vyombo vya habari ili kuimarisha uchumi wa tasnia hiyo.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema kuwa sekta ya habari inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kupungua kwa mapato pamoja na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani. Amesema hali hiyo imeongeza wasiwasi kwa wanahabari, pamoja na kuwepo kwa maoni kutoka kwa wadau wanaodai kuwa bado kuna sheria zinazokwaza uhuru wa vyombo vya habari.
Aidha, amesema kuwa mijadala imebaini kuwa uhuru wa vyombo vya habari una uhusiano wa moja kwa moja na hali ya uchumi wa vyombo hivyo. Amesema chombo cha habari kinapokuwa na uhuru wa kifedha, kina uwezo mkubwa wa kufanya kazi zake kwa uhuru bila shinikizo.
Hata hivyo, amesema ni muhimu kwa vyombo vya habari kutafuta vyanzo mbadala vya mapato badala ya kutegemea matangazo pekee. Amesema pia wanahabari hawapaswi kuikimbia teknolojia bali wanapaswa kuijifunza na kuitumia kuongeza ufanisi. Amesema AI si tishio bali ni nyenzo muhimu endapo itatumika kwa usahihi.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa MISA Kusini mwa Afrika Tanzania, Edwin Soko, amesema kuwa wadau wameendelea kujadili kwa kina hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini. Amesema tayari kulifanyika uchunguzi kupitia tume maalum iliyoundwa na serikali, pamoja na kuwasilishwa kwa ripoti kwa mamlaka husika ikiwemo kwa Rais.
Aidha, amesema ripoti hiyo ina mapendekezo muhimu yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha mazingira ya utendaji wa vyombo vya habari. Amesema ni muhimu kwa serikali kujenga uhusiano mzuri na wanahabari pamoja na kutambua uandishi wa habari kama taaluma rasmi.
Hata hivyo, ameonya kuwa si sahihi kwa watu wasiokuwa wanahabari kuwahukumu wanataaluma hao bila kuzingatia misingi ya taaluma hiyo. Amesema endapo mwanahabari atafanya makosa, anapaswa kushughulikiwa kupitia taasisi husika badala ya kuhukumiwa nje ya utaratibu.


No comments:
Post a Comment