![]() |
| Mkurugenzi wa LHRC, Wakili Dk Anna Henga |
![]() |
| Mratibu wa Utafiti wa LHRC, Wakili Fundikira Wazambi |
Mwandishi wetu, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Matukio ya Ukiukwaji wa Haki za Binaadamu Nchini, ikiwepo mauwaji, utekaji, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kukusanyika , kujichukulia sheria mkononi kwa wananchi yameongezeka kwa kiasi kikubwa na "kutia doa" Taifa la Tanzania.
Hayo yamebainishwa katika ripoti ya hali za haki za binaadamu 2025, ambayo imetolewa leo April 20, 2026 na Kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC) na Shirika la Zanzibar Fighting Against Youth Challenge Organization (ZAFAYCO),
Akisoma ripoti hiyo, Mratibu wa Utafiti wa LHRC, Wakili Fundikira Wazambi amesema, miongoni mwa matukio makubwa ya ukiukwaji wa haki za binaadamu, yaliyotokea mwaka jana ni vurugu za uchaguzi mkuu, ambapo mamia ya watu waliuawa, wengine kujeruhiwa, wengine kukamatwa na mali nyingi kuharibiwa.
Wakili Wazambi pia alisema kwa mwaka jana pia kimekuwepo na ongezeko la matukio ya utekaji ambapo watu 197 kwa kipindi cha miaka mitano waliliripotiwa kutekwa huku idadi kubwa ikiwa ni mwaka jana.
Amesema pia mwaka jana, kumekuwepo na matukio ya kuminya uhuru wa vyombo vya habari, kufungwa inteneti, kufungwa mitandao ya kijamii, kuingiliwa uhuru wa kuabudu ikiwepo kufungwa makanisa ya ufufuo na uzima na kuingiliwa uhuru wa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi wa LHRC, Wakili Dk Anna Henga amesema Machafuko yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi yaliibua hisia na wasiwasi mkubwa kuhusu ulinzi wa haki za msingi za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi na haki ya kukusanyika kwa amani.
Amesema ripoti ya hali ya haki za binaadamu mwaka jana, inaonesha ongezeko la matukio ya utekaji na upoteaji wa watu, ambapo LHRC ilikusanya matukio 80 mwaka 2025, yakihusisha wanasiasa na wananchi wa kawaida.
Wakili Dk Henga pia amesema kulikuwepo na ukiukwaji wa haki za kidigitali ikiwemo uminyaji na uzimaji wa internet na upatikanaji wa majukwaa ya mtandaoni wakati wa kipindi cha uchaguzi, hali iliyodhoofisha uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa.
Taarifa kamili ya ripoti ya hali ya haki za binaadamu mwaka 2025 itapatikana hapa.
https://humanrights.or.tz/en/post/resources-center/thrr2025


No comments:
Post a Comment