![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru |
![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru akizungumza na Mwenyekiti wa Taifa JOWUTA Mussa Juma na baadhi ya waandishi wa habari ofisini kwake mapema leo |
Mwandishi wetu,Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeng'arisha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya wafanyakazi duniani, Mei Mosi ambayo yatafanyika mkoani Njombe, kwa kuwezesha kampuni 16 za kilimo cha parachichi na viazi, kupata masoko nchini China, huku pia ikitarajiwa kuanza ujenzi wa Maabara ya kupima ubora wa mazao hayo mkoani Njombe.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mei mosi mwaka huu, mkoani Njombe na tayari, Mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka ametangaza mkoa huo kujiandaa vyema kwa maadhimisho hayo.
TPHPA inatarajia katika sehemu ya maadhimisho hayo, kuwekwa jiwe la msingi Jengo la Maabara ya mazao ya kimkakati Mei Mosi, hatua ambayo inatarajiwa kuwanufaisha maelfu ya wakulima wa mazao ya parachichi, Viazi mviringo na mengine, kupata hati za ubora wa mazao yao kwa ajili ya masoko ya kimataifa mkoani Njombe badala ya kuyasafirisha kwenda maeneo mengine ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru akizungumza na Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma pamoja na wanachama wa JOWUTA Leo, alisema Mamlaka hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wakulima na wafanyakazi nchini wananufaika na kilimo cha mazao ya kimkakati.
Profesa Ndunguru kwa sasa wamewezesha usajili wa makampuni 16 ya mazao ya kimkakati kupata masoko nchini China lakini pia mkakati wa kusaidia wakulima wengine unaendelea katika mikoa ya nyanda za juu kusini.
"Tunawasaidia wakulima kuweza kuuza bidhaa zao nje ya nchi, kwa kuzipima na kuziondolea mabaki ya viatilifu vyovyote ambavyo vinawezakuwa kubaki katika mazao yao"alisema
Alisema katika kuendeleza kazi hiyo, Mamlaka hiyo, itaanza karibuni ujenzi wa maabara katika mji wa Makambako ambayo itasaidia sana hata wakulima wadogo wadogo kupata masoko ya uhakika nje ya nchi.
Akizungumzia maadhimisho ya Mei Mosi, Ndunguru alisema Mamlaka hiyo kama ilivyokawaida itashiriki ipasavyo katika ngazi mbali mbali hadi taifa na itashirikiana na JOWUTA kuhakikisha inatimiza wajibu wake, ikiwepo kuhabarisha umma kazi nzuri ambazo zinafanywa na Serikali.
Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma akizungumza na Mkurugenzi huyo, alimpongeza kwa kazi nzuri ambayo TPHPA wamekuwa wakifanya ambayo sasa inahakikisha usalama walaji wa mazao mbali mbali ambayo yanazalishwa hapa nchini na wakulima
"TPHPA inafanyakazi kubwa na sisi wanahabari tunawapongeza kwa sababu mmeweza kudhibiti kuingia nchini viatilifu visivyo na ubora, mmekuwa mkiwasaidia wakulima kuzingatia afya zao na walaji katika matumizi ya viatilifu, kuwasaidia kupata masoko ya uhakika nje ya nchi lakini pia mmekuwa mkisaidia tafiti nyingi za masuala ya afya ya mimea na vyakula"alisema
Juma alisema JOWUTA mwaka huu itashiriki maadhimisho na Mei mosi kwa mara ya kwanza baada ya kujiunga na shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na inatarajiwa kutoa wafanyakazi bora katika sekta ya habari.
MWISHO



No comments:
Post a Comment