Mwandishi wetu, Kilimanjaro
maipacarusha20@gmail.com
Moshi. Katika kuadhimisha Siku ya Dunia (Earth Day), wadau wa utalii mkoani Kilimanjaro wameungana kupanda miti ikiwa ni juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame mkubwa mwaka jana.
Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Mauly Tours, Sharifa Mauly, amesema ukame ulioshuhudiwa mwaka uliopita uliathiri kwa kiasi kikubwa mazingira, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, ambao ni tegemeo muhimu la kiikolojia na kiuchumi.
Amesema ni muhimu kwa jamii kuacha tabia ya ukataji wa miti ovyo na badala yake kuongeza juhudi za upandaji miti ili kurejesha uoto wa asili uliopotea kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha upatikanaji wa maji unaimarika.
“Tunatoa wito kwa shule na jamii kwa ujumla kuendelea kuotesha miti. Leo tumepanda miti 200 ya kivuli na matunda, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha uoto wa asili katika maeneo yetu,” amesema Sharifa.
Aidha, ameipongeza serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa hamasa na kuunga mkono juhudi za upandaji miti nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Uru Community, Gift Simle, amesema upandaji miti shuleni hapo ni sehemu ya jitihada za kukuza uelewa wa wanafunzi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
Amesema licha ya athari za mabadiliko ya tabianchi kuonekana wazi, bado kuna juhudi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo.
“Upandaji miti utatusaidia kupata matunda, hewa safi na kuboresha mazingira yetu. Tukichunguza hali ya Mlima Kilimanjaro, tunaona wazi miti inakatwa, jambo ambalo likiendelea linaweza kusababisha kupungua kwa barafu katika mlima huo,” amesema Simle.
Naye mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo, Erick Lucas, amesema maadhimisho ya siku ya dunia yamewasaidia wanafunzi kuelewa umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
“Tunafurahi kushiriki upandaji miti kwani unatupa elimu na hamasa ya kutunza mazingira. Miti inatusaidia kupata hewa safi na lishe kupitia matunda,” amesema Erick.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment