Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
RAIS wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, amesema kuwa Serikali inapoendelea kusikiliza na kushirikiana na wachimbaji wadogo, inasaidia kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha sekta ya madini inanufaisha pande zote.
Kauli hiyo aliitoa katika kikao kilicholenga kujadili na kusikiliza changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini mkoani Morogoro.
Bina alisema ni wajibu wa wachimbaji na wadau wote wa sekta ya madini kuungana, kushirikiana na kuwa na sauti moja ili kufikia maendeleo ya pamoja.
“Sisi wachimbaji ni sehemu muhimu ya uchumi wa nchi, hivyo ushirikiano huu unaendelea kutuweka pamoja na kusaidia kuboresha mazingira ya kazi yetu,” alisema.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wachimbaji kutafakari walipo na wanapoelekea, ili kuelewa mwelekeo wao na kufanya maamuzi sahihi yatakayowafikisha kwenye maendeleo endelevu ya sekta ya madini.
Kutokana na hali ilivyo sasa, Bina alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kuanzia ngazi ya chini hadi viongozi wa vyama na mashirikisho, pamoja na kufanya vikao vya mara kwa mara kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua.
Takwimu zinaonesha kuwa mwitikio wa wachimbaji wadogo katika kutumia huduma za kifedha bado ni mdogo, kutokana na changamoto za uelewa na uaminifu kwa taasisi za kifedha.
Hata hivyo, alisema jitihada zilizofanywa katika sekta ya madini, ikiwemo kuhamasisha upatikanaji wa mitaji, zimeanza kuzaa matunda, ambapo wachimbaji wengi wameanza kuona umuhimu wa kukopa ili kukuza shughuli zao. Serikali imeendelea kushirikiana na mabenki ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji.
Alisisitiza kuwa ili kukuza uchumi na kufikia mafanikio makubwa, wachimbaji wanapaswa kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na taasisi za kifedha, akibainisha kuwa wachimbaji wengi sasa wameanza kukopa kwa kasi kubwa.
Kwa mujibu wa takwimu, mwaka jana mabenki yalitoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 160 kwa wachimbaji. Hata hivyo, bado kuna pengo kwa wachimbaji wadogo ambao hawajatumia ipasavyo fursa hizo.
Bina aliwashauri wachimbaji wadogo kujiunga katika vikundi ili kuongeza sifa za kupata mikopo, kwani kupitia mfumo huo hata wasiokuwa na dhamana binafsi wanaweza kunufaika.
“Baadhi ya mabenki tayari yanaonyesha utayari wa kutoa mikopo kwa wachimbaji, jambo linaloashiria fursa kubwa iliyopo katika sekta ya madini,” alisema.
Aliwataka wachimbaji kuchangamkia fursa hizo ili kuboresha uzalishaji na kuinua kipato chao.
Kwa upande wao, baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini mkoani Morogoro waliomba Serikali kuwekeza zaidi katika kuongeza thamani ya madini, ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya migodi.
Mchimbaji mdogo, Benald Nduguru, alisema Morogoro ni mkoa wenye rasilimali muhimu za madini, ikiwemo madini ya ujenzi na viwandani, hivyo kuna haja ya kuwawezesha wachimbaji na kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Morogoro (MOREMA), Dk. Omary Mzeru, aliomba Serikali kuwapatia eneo lililofutwa ili chama hicho kiweze kuwekeza na kuwakaribisha wawekezaji wengine.
Aidha, Dk. Mzeru aliwataka wanachama kutumia chama chao kufikisha changamoto na malalamiko yao badala ya kusubiri vikao, ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Morogoro, Zabibu Napacho, aliahidi kuwaunganisha wachimbaji wa mkoa huo na kushughulikia changamoto zilizopo.
Napacho alisema ofisi yake ina jukumu la kusimamia Sheria ya Madini, hivyo baada ya kupokea kero na migogoro, huhakikisha inafuatwa sheria na kushirikiana na wahusika ili kutatua matatizo hayo.
Kwa upande mwingine, Rais wa FEMATA, John Bina, aliwasihi wachimbaji kutambua thamani ya madini nchini kwa kufuata taratibu na sheria za uchimbaji.
...

No comments:
Post a Comment