SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA TARSI KATIKA KUIMARISHA USALAMA BARABARANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 24 April 2026

SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA TARSI KATIKA KUIMARISHA USALAMA BARABARANI

 




Na Queen Lema,Arusha 


maipacarusha20@gmail.com 


Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imepongeza juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Mpango wa Usalama Barabarani (TARSI) katika kuimarisha taaluma ya uhandisi na kupunguza ajali za barabarani nchini kupitia mafunzo kwa wataalamu mbalimbali.

Akifungua mafunzo ya siku tatu yanayowakutanisha wahandisi kutoka maeneo tofauti nchini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Riziki Shemdoe, alisema serikali inaipa kipaumbele sekta ya uhandisi hasa katika kuhakikisha miundombinu ya barabara inakuwa salama zaidi kwa watumiaji wote.

Alisisitiza kuwa mafunzo ya mara kwa mara kwa wahandisi ni muhimu katika kuongeza ubunifu na ufanisi wa kazi zao, jambo litakalosaidia kupunguza ajali zinazotokana na changamoto za miundombinu.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TARSI, Maliki Barongo, alieleza kuwa taasisi hiyo inaendelea kujikita katika kutoa elimu na kufanya tafiti zinazolenga kupunguza ajali za barabarani, huku akihimiza wadau kushirikiana ili kufikia malengo ya pamoja.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka Taasisi ya Mifupa (MOI), Dkt. Joel Bwemelo, alieleza kuwa ajali nyingi zinaweza kuepukika iwapo watumiaji wa barabara watazingatia kanuni za usalama, huku akisisitiza umuhimu wa tahadhari ili kupunguza madhara yatokanayo na ajali.

Aidha, Laurent Maganga kutoka Norplan Tanzania alipendekeza kuingizwa kwa masuala ya usalama barabarani katika mitaala ya uhandisi ili kuwaandaa wahandisi wenye uelewa mpana wa usalama tangu wakiwa vyuoni.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wahandisi kwa kuwapatia mbinu bora na kuwapa nafasi ya kubadilishana uzoefu, hatua inayotarajiwa kuchangia kuboresha ubora wa barabara na kupunguza ajali zinazotokana na mapungufu ya miundombinu.

No comments: