Wamiliki wa visima vya maji ya chini ya ardhi wapewa siku saba kulipia ada - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 21 April 2026

Wamiliki wa visima vya maji ya chini ya ardhi wapewa siku saba kulipia ada




Burhani Yakub Tanga


maipacarusha20@gmail.com 

Wamiliki wa visima vya Maji wa Wilaya ya Tanga wamepewa siku saba kuhakikisha wanalipia leseni ya matumizi ya maji ya chini ya ardhi ili mapato ya Serikali yasipotee.


Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Segule Segule ametoa amri hiyo leo baada ya kufanya ukaguzi wa visima vya Maji vilivyopo katika Wilaya ya Tanga na kubaini upotevu wa mapato ya Serikali kutokana na baadhi ya wamiliki kutokuwa na leseni za matumizi ya maji.


Amefanya ukaguzi huo kufuatia wataalamu wa Bodi hiyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga pamoja na Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) kuendesha mradi wa Green Cities)unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la ujerumani GAZ.


Kupitia mradi huo,Bodi hiyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga pamoja na Tanga Uwasa wanaendesha tathmini ya utambuzi wa visima vilivyopo,kujua takwimu za ubora wa maji na uwingi wake.


"Kuna baadhi ya wamiliki wa visima vya maji hawana leseni za matumizi ya maji wanadhani walipopewa leseni za uchimbaji ndiyo wamemaliza...tumewapa elimu kwamba sheria inawalazimu kila mwaka kukata leseni ya matumizi ambayo ni sh 300,000 na nimewapa siku saba wasipotekeleza hatua dhidi yao zitachukuliwa,hatuwezi kukubali mapato ya Serikali kupotea kiasi hicho"amesema Segule.


Akiwa katika ukaguzi huo, Mkurugenzi huyo alyembatana na wataalamu wa maabara,wahandisi wa ujenzi wa visima vya maji ya chini ya ardhi pamoja na maafisa kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga waliweza kupima ubora wa maji na uimara wa visima vilivyojengwa katika maeneo mbalimbali vikiwamo vinavyomilikiwa na shule,zahanati, vituo vya afya,nyumba za ibada na wamiliki binafasi wanaoesha biashara za kufuatua matofali,viwanda na makazi.


Baadhi ya wamiliki wa visima vya maji
walioizungumza na mwandishi wa habari hizi wamesema wapo tayari kulipia leseni kama walivyoelekezwa kwa kuwa wananufaika na maji hayo.


"Kesho tutakwenda ofisi za Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani kupata utaratibu wa namna ya kulipia leseni za matumizi kwa kuwa maji haya yanatudaidia sana kuendesha shughuli zetu za kufuatua matofali"amesema Joseph Samwel wa kampuni ya Katemi Enterprises.


Afisa Mtendaji wa mtaa wa Saruji,Fahad Salumu amesema tathmini hiyo imeawezesha kutambua idadi ya visima vya maji ya chini vilivyopo katika eneo lake ubora na takwimu nyingine zinazohusiana na maji.


Mkaguzi wa ubora wa maji kutoka maabara ya Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani,Mpajieli Joseph amesema hadi sasa wameshachukua sampuli 30 katika visima vilivyopo maeneo ya jamii ambazo zitafanyiwa uchunguzi wa kina zaidi.


"Kwa mfano katika shule ya Sekondari Maweni katika vipimo vya awali tumebaini maji yake yanafaa kwa matumizi ya binadamu ikiwamo kuyanywa lakini tumechukua sampuli ili kupeleka kwenye maabara yetu kuu kwa uchunguzi zaidi"amesema Nice Ninja ambaye ni mtaalamu wa maji ya chini kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani.


Hata hivyo mtaalamu huyo amesema taarifa rasmi kuhusu tathmini nzima ya utafiti unaoendelea itatolewa mara baada ya mradi huo kufikia tamati.


MWISHO

No comments: