Wanachama, Kirua Vunjo North Walalamikia ‘Kutoweka’ kwa Sh5 Milioni za Mauzo ya Trekta - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 23 April 2026

Wanachama, Kirua Vunjo North Walalamikia ‘Kutoweka’ kwa Sh5 Milioni za Mauzo ya Trekta




Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Kirua Vunjo North, Heriel Ngowi akizungumza na wananchi katika mkutano huo












Na Mwananchi wetu, Moshi




maipacarusha20@gmail.com




Moshi. Wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika Kirua Vunjo North, mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia upotevu wa fedha zinazodaiwa kupatikana baada ya kuuzwa kwa trekta la chama hicho, wakitaka serikali iingilie kati ili haki itendeke.




Akizungumza katika mkutano mkuu wa kufungua msimu wa kilimo wa mwaka 2026/2027 uliofanyika jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Heriel Ngowi, alisema trekta hilo liliondolewa katika mazingira yasiyoeleweka na baadaye kuuzwa kama chuma chakavu.




“Baada ya trekta na tela kuondoka, ikafika wakati likakatwa kama chuma chakavu na inadaiwa liliuzwa kwa Sh5 milioni. Hadi leo fedha hizo hazijulikani zilipo,” alisema Ngowi, akirejea maamuzi ya mkutano wa Mei 11, 2022 uliotaka fedha hizo zirejeshwe.




Aliongeza kuwa trekta hilo lilikuwa na usajili wa serikali na lilimilikiwa kwa pamoja na vyama viwili, lakini baada ya changamoto za uzalishaji wa zao la kahawa, ushirika uliendelea kama chama kimoja kabla ya kuuzwa kwa trekta hilo.




Baadhi ya wanachama, akiwemo mkulima wa kahawa, Averini Kilawe, walieleza kutoridhishwa na mchakato mzima wa uuzaji huo, wakidai haukuwa wazi wala kuwashirikisha wanachama ipasavyo.




Kwa upande wake, Stanislaus Marenge alisema ingawa wanachama walikubaliana trekta liuzwe baada ya kukaa muda mrefu bila kutumika, utekelezaji wake uliibua sintofahamu.




“Tulikubaliana liuzwe, lakini hatujui liliuzwaje wala fedha zake zilipo,” alisema Marenge.




Naye Felix Mallya alidai uuzaji huo ulifanyika kwa siri na kwa bei ya chini tofauti na thamani halisi ya trekta hilo.




“Trekta liliuzwa kinyemela kwa Sh5 milioni, lakini cha kushangaza hadi sasa hakuna hata shilingi tano iliyoonekana. Inaonekana viongozi waliokuwepo walihusika na fedha hizo,” alidai Mallya.




Wanachama hao walisema suala hilo limeendelea kuwa kikwazo kwa maendeleo ya chama, wakieleza kuwa linadhoofisha juhudi za wakulima katika kuinua sekta ya kahawa.




Katika mkutano huo, walisisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi waadilifu na wenye hofu ya Mungu ili kuhakikisha rasilimali za chama zinasimamiwa kwa uwazi na ufanisi.




Aidha, walitoa wito kwa serikali kuchunguza sakata hilo na kuhakikisha fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya trekta hilo zinarejeshwa kwa manufaa ya wanachama na maendeleo ya kilimo katika eneo hilo.




Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, Jackline Senzige, alisema tayari alishatoa maagizo kwa uongozi uliokuwepo kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.




“Niliagiza viongozi waliokuwepo kipindi hicho, nadhani mwaka 2022, kuhakikisha fedha hizo zinarudi kwenye chama. Hadi sasa sijapata taarifa rasmi kama fedha hizo zimerejeshwa,” alisema Senzige.




Mwisho..

No comments: