Wapelekeni wasichana shule zenye maadili -Sheikh Farhat - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 20 April 2026

Wapelekeni wasichana shule zenye maadili -Sheikh Farhat









Burhani Yakub, Tanga.


Ukatili wa kingono limetajwa kuwa janga katika malezi ya wasichana kutokana na utandawazi pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii iliyoiteka jamii katika siku za hivi karibuni.


Mkuu wa dawati la kupinga ukatili wa kijinsia katika jeshi la polisi Wilaya ya Tanga mjini, Neema Ndorosi ametoa taarifa hiyo wakati wa mahafali ya 16 ya kuwaaga wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya Sekondari ya kiislamu ya Wasichana ya Al- Kheir iliyopo Jijini Tanga.


Amesema miongoni mwa matukio ya ukatili wa kingono ni pamoja na wasichana kujipiga picha zisizofuata maadili na kwa kujua au kutojua baadaye zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii.


"Msipige picha zisizofuata maadili unaweza kukuta simu yako inachukuliwa na mtu mwenye nia mbaya akiperuzi na kuziona anazisambaza kwenye mitandao ya kijamii hatimaye tumeshuhudia wasichana baadhi yao wakijidhuru kwa sababu ya fedheha anayoipata"amesema Neema


Amesema matukio ya ukatili wa kingono ni janga ambalo linahitaji jamii ipambane nao kwa sababu una madhara makubwa katika suala zima la malezi.


Mkuu wa shule hiyo,Sheha Hamad Sheha amesema jumla ya wanafunzi 32 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita mwezi Mei 2026 ya tahasusi za PCB,CBG,HGL,HKL,HGE,HGK,ECA na mfunzo ya elimu ya dini ya kiislamu.


Amesema tangu kuanzishwa kwa masomo ya elimu ya Sekondari ya juu mwaka 2010 wahitimu wote 279 katika shule ya Al Kheir wamefaulu kwa madaraja ya kwanza hadi tatu na kujiunga na vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi wakisomea fani za sheria,elimu,famasia,udaktari,ukandarasi na tehama.


Mkurugenzi wa taasisi ya kimataifa ya Direct Aid Society -Tanga,Sheikh Ahmed Farhat amewahimiza wazazi wanapotafuta shule za kuwapeleka watoto wao mbali ya taaluma wazingatie shule zenye kufundisha malezi bora na maadili mema.


"Katika kipindi hiki ambacho tunashuhudia mmomonyoko wa maadili Kwa vijana,wazazi wanapaswa mbali ya taaluma wazingatie shule zenye kufundisha malezi bora na maadili mema kama hapa Al-Kheir."amesema Farhat.


Katika mahafali hayo wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili wa shule hiyo walifanya maonesho ya masomo ya sayansi likiwamo na kuelezea saratani ikiwamo ya ngozi inavyochangiwa na matumizi ya vipodozi na ulaji usiofuata mpangilio wa vyakula


MWISHO

No comments: