ADHABU YA VIBOKO MASHULENI UNAATHIRI KIHISIA NA KISAIKOLOJIA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 2 May 2026

ADHABU YA VIBOKO MASHULENI UNAATHIRI KIHISIA NA KISAIKOLOJIA



 Na Mwandishi Wetu, maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


WAKATI  Dunia inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Adhabu za Viboko, huku mashirika ya kiraia yanayotetea haki za mtoto yakibainisha kuwa hali bado ni tete nchini Tanzania, ambapo takribani asilimia 70 ya watoto wameathirika kihisia na kisaikolojia kutokana na ukatili wa vipigo katika makuzi yao.


Kauli hiyo imetolewa na wadau wa haki za binadamu wakionya kuwa licha ya maadhimisho hayo ya kimataifa ambayo hufanyika kila mwaka Aprili30, bado jamii inahitaji kuchukua hatua madhubuti kulinda ustawi na haki za watoto


“Walimu ni miongoni mwa wahusika wanaoripotiwa mara nyingi katika mazingira ya shuleni kwa kutoa adhabu ya viboko”alisema Angela.


Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Kukomesha Adhabu za Viboko nchini na Mkurugenzi wa Shirika la Save the Children Tanzania, Angela Kauleni, amesema hali hiyo inaonyesha kuwa bado jamii inahitaji uelewa mpana kuhusu madhara ya adhabu hizo.


Amesema takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa kati ya watoto watau hadi wane duniani wenye umri wa miaka 2 hadi 14 hukumbwa na aina fulani ya ukatili kila mwaka, huku adhabu za viboko zikichangia kwa kiwango kikubwa hususan majumbani.


“Adhabu za viboko zinadhoofisha utu wa mtoto, zinaharibu afya ya akili na haziwasaidii watoto kujifunza nidhamu kwa ufanisi. Tunahitaji kubadilisha mtazamo na mbinu za malezi na ufundishaji,” amesema Kauleni.


Alieleza kuwa, adhabu hizo bado zinatumika katika mazingira mbalimbali ikiwemo shule, madrasa na majumbani, licha ya ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa haziboresha tabia wala kuongeza ufaulu wa wanafunzi.


Alisema tafiti zinaonyesha kuwa adhabu ya viboko husababisha hofu,kujitenga,kupungua kwa ushiriki,kushuka kwa ufaulu wa masomo pamoja na madhara ya muda mrefu ya kihisia na kisaikolojia.


Naye Mkurugenzi wa ulinzi wa mtoto kutoka  UNICEF Tanzania, Miranda Armstrong, amesema hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa adhabu za viboko zina mchango chanya katika kujenga nidhamu, bali zinachochea hofu, msongo wa mawazo na hata kuacha shule kwa baadhi ya watoto.


Mashirika hayo yametoa wito mahsusi kwa serikali kuchukua hatua za haraka kurekebisha sheria ili kupiga marufuku adhabu za viboko katika mazingira yote, ikiwemo shule na majumbani, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa sera za ulinzi wa mtoto.


Aidha, yametaka walimu kupewa mafunzo ya mbinu mbadala za nidhamu chanya, wazazi kuelimishwa kuhusu malezi yasiyo ya ukatili, na viongozi wa dini na jamii kushiriki kikamilifu katika kupinga mila na desturi zinazochochea ukatili dhidi ya watoto.


Vyombo vya habari navyo vimetakiwa kuongeza juhudi za kuelimisha umma kuhusu madhara ya adhabu za viboko na kuhamasisha mabadiliko ya mitazamo ya kijamii.


Mashirika hayo yamesisitiza kuwa kukomesha adhabu za viboko siyo kuondoa nidhamu, bali ni kujenga mfumo bora wa malezi unaolinda utu, haki na mustakabali wa mtoto


Akitolea mfano tukio la mwaka 2025: Mkurugenzi wa Elimu kwa umma na ufuatiliaji wa haki za binadamu(LHRC) Wakili Deogratius Bwire,mkoani Shinyanga mahakama kuu ilitoa hukumu ya kesi ya mtoto kutoka katika shule moja wapo aliyepigwa viboko 10 ambavyo vilipelekea kupoteza fahamu (kuzimia) na wakati akikimbizwa hospital umauti ulimfika akiwa njiani.


“Mtoto huyu alikua wakike, kosa ni kutokufanyakazi kwa ufasaha iliyokua imetolewa na mwalimu wa somo la jeographia,ni wakati sasa wa serikali kupitia sharia za elimu na miongozo upya ilikuonndoa adhabu hii ya viboko shuleni”alisema wakili Bwire.


Taarifa hiyo ilitolewa kwa pamoja na mashirika mbalimbali yakiwemo  Save the Children Tanzania, WiLDAF, HakiElimu, Zanzibar Child Rights Forum (ZCRF), Zanzibar Female Lawyers Association (ZAFELA), Shule Direct, Children’s Dignity Forum (CDF), Tanzania Child Rights Forum (TCRF), Msichana Initiative, Legal and Human Rights Centre (LHRC), FAWE Tanzania, ZAPHA+, Zanzibar Legal Aid and Human Rights Organization (ZALHO), Tanzania Media Women Association (TAMWA), Christian Social Services Commission (CSSC), pamoja na UNICEF yakisisitiza umuhimu wa hatua za haraka kukabiliana na tatizo hilo.


Mwisho.

No comments: