![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga akimkabidhi cheti mfanyakazi Bora wa Kampuni ya MATI Super Brands LTD |
maipacarusha20@gmail.com
Kampuni ya MATI Super Brands LTD yenye makao yake makuu mjini Babati mkoani Manyara, imeibuka mshindi wa kwanza kwa kutwaa tuzo katika vipengele vitatu, vikiwemo Tuzo ya Banda Bora la Maonesho pamoja na Ushindi wa Jumla wa Maonesho ya Mei Mosi Mkoa wa Manyara.
Kampuni hiyo yenye kampuni tanzu za MATI Foundation, MATI Zoo na MATI LTD South Africa, imeweka historia kwa kuvunja rekodi ya ushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka 2026 yaliyofanyika katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, ngazi ya Mkoa wa Manyara, baada ya kuingia na msafara mkubwa wa magari uliovutia hisia za wengi.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, amewapongeza wawekezaji wa mkoa huo akisema MATI Super Brands LTD ni mfano bora wa mwekezaji kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani hapo.
![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga akiweka Saini kwenye kitabu Cha wageni alipotembelea Banda la MATI Super Brands LTD |
“Niwatie moyo wawekezaji wote wa Mkoa wa Manyara kwamba serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuinua uchumi wa wananchi. MATI Super Brands LTD wamekuwa wawekezaji wazuri katika mkoa wetu. Nimeona magari mengi leo kwenye maandamano, madereva wanaoendesha ni miongoni mwa wafanyakazi waliopata ajira katika kampuni hii,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji wenye nia njema ili kuchochea maendeleo ya Tanzania kwa ujumla.
MATI Super Brands LTD ni mwajiri wa wafanyakazi zaidi ya 1,000 nchini Tanzania pamoja na ukanda wa nchi za Maziwa Makuu na Afrika Kusini
MATI Super Brands LTD ni wazalishaji wa vinywaji changamshi vya aina mbalimbali vinavyopatikana sokoni ndani na nje ya Tanzania, ikiwa ni moja ya makampuni yanayokua kwa kasi katika sekta hiyo.
![]() |
Vinywaji hivi vimejipatia umaarufu kutokana na ubora wake, ladha zake tofauti na upatikanaji wake mpana katika maeneo mbalimbali ya biashara.
Aidha, kampuni hiyo pia huzalisha bidhaa nyingine kama Tanzanite Premium Vodka, Tanzanite Royal Gin na Jax’s Will Premium Whiskey, ambazo zimeendelea kuimarisha nafasi yake katika soko la vinywaji changamshi.
MATI Super Brands LTD imejijengea heshima kama mzalishaji muhimu anayechangia ukuaji wa sekta ya viwanda na uchumi kupitia bidhaa zake zinazozalishwa kwa viwango vya ushindani.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa MATI Super Brands LTD, Bw. David Mulokozi, ambaye ni mwekezaji wa ndani mzawa, amesema Tanzania ni eneo huru, lenye amani na salama kwa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Amesema mazingira mazuri ya biashara pamoja na fursa nyingi za kiuchumi zilizopo nchini yanaendelea kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, utalii, kilimo na huduma.
Bw. Mulokozi ameweka bayana dhamira yake ya kuendelea kukuza uchumi wa Tanzania kupitia sekta za viwanda, utalii na hifadhi ya mazingira, huku akiwahamasisha wawekezaji wengine kutumia fursa zilizopo nchini kwa maendeleo ya taifa.
Sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari na Siku ya Wafanyakazi Duniani, Bw. David Mulokozi na kampuni yake ya MATI Super Brands LTD wameonesha mshikamano na vyombo vya habari kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini (RUJAT) ili kuhakikisha habari za vijijini pamoja na sauti za pembezoni zinapewa kipaumbele katika vyombo vya habari nchini Tanzania.







No comments:
Post a Comment