Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ndege maalum aina ya Boeing 787-8 Dreamliner kwenda Morocco kwa ajili ya kuisafirisha Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U17), utakaochezwa Juni 2, 2026 nchini Morocco.
Hii ni hatua kubwa ambayo haijawahi kufikiwa na timu yoyote ya vijana chini ya miaka 17 nchini, na inaonesha maendeleo makubwa ya soka la vijana Tanzania.
Mbali na kufuzu fainali, Serengeti Boys pia wameweka rekodi nyingine ya kihistoria kwa kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la U17, linalotarajiwa kufanyika nchini Qatar mwezi Novemba 2026.
Akizungumza leo Mei 29, 2026 jijini Dodoma, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba amesema Serikali imejipanga kuhakikisha timu hiyo inapewa sapoti ya kutosha kuelekea mchezo wa fainali.
Amesema Rais Samia pia ametoa Sh500 milioni kwa kikosi kizima cha Serengeti Boys pamoja na benchi la ufundi kama pongezi kwa kufika hatua ya fainali.
Aidha, amesema endapo timu hiyo itafanikiwa kutwaa ubingwa, kila mchezaji na viongozi wa benchi la ufundi watapatiwa kiwanja katika eneo la Suluhu New City mkoani Morogoro.
Waziri Mkuu huyo ameielekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuratibu safari ya wadau mbalimbali wa michezo, viongozi wa wizara, Shirikisho la Mpira wa Miguu na wabunge, kwenda Morocco kwa ajili ya kuwapa hamasa vijana hao.
“Tunaamini kwamba, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ametoa ndege kubwa aina ya Dreamliner, tutakuwa na nafasi ya kubeba kombe na watu wa kwenda kuwapa chachu vijana wetu ili warudi na kombe,” amesema.

No comments:
Post a Comment