SUKARI TANZANIA YANOGA KWA TEKNOLOJIA YA KIDIJITALI KUPIGA VITA UDANGANYIFU NA KUIMARISHA UZALISHAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 18 May 2026

SUKARI TANZANIA YANOGA KWA TEKNOLOJIA YA KIDIJITALI KUPIGA VITA UDANGANYIFU NA KUIMARISHA UZALISHAJI

 



Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi,







Na Lilian Kasenene, Bagamoyo



maipacarusha20@gmail.com


Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi, amesema Serikali imeweka mifumo ya kidijitali yenye usalama wa hali ya juu inayosaidia kudhibiti udanganyifu katika sekta ya sukari, hususan kwenye mikopo ya wakulima na vibali vya uagizaji wa sukari.


Alisema hayo wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, wakati wa kongamano la wataalamu wa miwa na sukari kutoka viwanda, vyuo, bodi na taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta hiyo nchini.

Picha ya pamoja


Prof. Bengesi alieleza kuwa kupitia mifumo hiyo, benki sasa zinaweza kumtambua mkulima halisi kwa kutumia namba ya usajili, ambapo mfumo huonyesha shamba lake moja kwa moja na hivyo kuondoa uwezekano wa udanganyifu kwenye mikopo.


“Siku za nyuma baadhi ya wakulima walitumia mwanya huo kudanganya, lakini sasa haiwezekani. Benki inapoingiza namba ya mkulima inaona shamba lake moja kwa moja. Fedha iko salama,” alisema.


Alibainisha pia kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yamepunguza kwa kiasi kikubwa udanganyifu katika vibali vya uagizaji wa sukari, kwani uhalali wake unaweza kuthibitishwa kwa haraka na kwa usahihi.

Wadau wa sukari

Aidha, alisema teknolojia ya kidijitali imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya sukari kuanzia shambani hadi viwandani, ikiboresha ufanisi wa uzalishaji na kupunguza mianya ya udanganyifu katika mnyororo wa thamani.


Aliongeza kuwa mifumo hiyo pia imeimarisha udhibiti wa uingizaji wa sukari feki na kuongeza uwazi katika biashara ya sukari nchini.


Kwa ujumla, Prof. Bengesi alisema sekta ya sukari ina fursa kubwa ya kukua kutokana na nafasi ya kijiografia ya Tanzania, masoko ya kikanda na maendeleo ya teknolojia, akisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika tafiti na mbinu bora za kilimo.


Alisema changamoto zilizopo katika sekta hiyo zimekuwa chachu ya ubunifu na utafiti unaosaidia kuleta suluhisho mbalimbali.


Rais wa Chama cha Wataalamu wa Sukari Tanzania (TSSCT), Fihiri Achi, alisema chama hicho kina jukumu la kuratibu na kuendeleza utaalamu katika mnyororo mzima wa uzalishaji wa sukari, kuanzia mashambani hadi viwandani.


Alieleza kuwa wanachama wake wanashirikiana kutafuta suluhisho la changamoto na kufanya tafiti zinazolenga kuongeza tija na kuboresha uzalishaji wa miwa na sukari.


Katika upande wa kilimo, alisema jitihada zinaendelea kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora kupitia vitalu vya mbegu vinavyolenga kuongeza ubora wa miwa na mavuno.


Aidha, alibainisha kuwa sekta hiyo inaendelea kuingia katika matumizi ya teknolojia za kisasa kama mashine za kuvuna, droni na mifumo ya kidijitali, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wakulima wadogo pia wananufaika.


Mkulima na mtaalamu wa kilimo cha miwa, Dk. George Mlingwa, alisema sekta ya sukari imepiga hatua kutokana na ushirikiano wa serikali, wakulima na taasisi mbalimbali za utafiti na maendeleo.


Alisema wakulima sasa wanapatiwa mafunzo ya kitaalamu ambayo yamewasaidia kuboresha mbinu za kilimo na kuongeza uzalishaji.


Aidha, alibainisha kuwa mbegu bora za miwa zilizotokana na utafiti zimeongeza mavuno kwa kiasi kikubwa, ambapo baadhi ya maeneo yamepanda kutoka tani 20 hadi zaidi ya tani 50 kwa ekari.


Meneja wa Umwagiliaji wa Kiwanda cha Sukari Bagamoyo, Alison Zahoro, alisema kiwanda hicho kinatumia mifumo ya kisasa ya umwagiliaji inayotoa maji moja kwa moja kwenye mizizi ya miwa na kuongeza tija ya uzalishaji.


Alisema pia kiwanda hicho kinashirikiana na jamii kupitia ajira, huduma za afya, visima vya maji na elimu kwa wananchi wa vijiji jirani.


Katibu wa TSSCT, Mwanaidi Jaffery, alisema sekta ya sukari inaendelea kujengewa uwezo wataalamu ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji.


Aliongeza kuwa ushiriki wa vijana katika sekta hiyo unaongezeka kupitia makongamano na ushirikiano na 

wakulima, jambo linalosaidia kuimarisha mustakabali wa sekta ya sukari nchini.


....

No comments: