Ukosefu wa chakula shuleni waathiri wanafunzi wa Longido,CORDS waja na Mradi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 16 May 2026

Ukosefu wa chakula shuleni waathiri wanafunzi wa Longido,CORDS waja na Mradi




Meneja miradi Elimu Cords Ezekiel Piniel


Mwandishi wetu, Longido


maipacarusha20@gmail.com 


Wanafunzi wa shule za Msingi wilaya ya Longido, wakiwepo wanafunzi wa MEMKWA ,wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwepo kukosa chakula shuleni, hali ambayo inaathiri maendeleo yao ya Kitaaluma na hivyo, kuibua wadau kadhaa wa elimu kuanza kusaidia.


Hayo yamebainisha katika kikao cha jukwaa la wadau wa Elimu wilaya ya Longido mkoa Arusha ,lililoandaliwa na  Shirika la  Utafiti,Maendeleo na Huduma za Jamii ( CORDS) na kuwashirikisha viongozi wa halmashauri ya Longido, waratibu elimu, viongozi wa vijiji , Walimu na Asasi za kiraia.

Mratibu Mradi elimu Cords

Akizungumza katika kikao hicho,Afisa Elimu wa Kata ya Ngarenaibo,Paulo Teveli alisema tatizo la wazazi kutopeleka chakula shuleni ni kubwa na linachangia kuzorotesha maendeleo ya wanafunzi.


Teveli alisema, hali hiyo, inatokana na baadhi ya wazazi kutothamini elimu lakini pia wengine kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.


"Tatizo  ni kubwa na linaathiri hadi wanafunzi wa MEMKWA ambao katika Kata yangu wapo 31 jambo ambalo tunapaswa tulishughulikie kwa kushirikiana wadau wote,lakini tunapongeza misaada  ambayo tumekuwa tukipata kutoka CORDS katika kusaidia sekta ya elimu"alisema

Mwalimu Sein Kitomari

Mwalimu Sein Kitomali wa shule ya Msingi Longido  alisema chakula shuleni ni moja ya changamoto kubwa kwa wanafunzi katika jamii za kifugaji ambapo bado kuna wazazi hawathamini elimu.


Kitomali ambaye anasimamia wanafunzi wa MEMKWA katika shule ya Msingi Longido, alisema wanafunzi wanatoka umbali mrefu kufika shule hivyo ni muhimu sana wawe na chakula cha uhakika na kupata vifaa vyote muhimu, ikiwepo sale na vifaa vya kujifunzia .


Alisema katika shule hiyo, kuna wanafunzi 62 wa MEMKWA  ambapo kati yao 38 wanajiandaa kwa mitihani ya darasa la nne mwaka huu na kueleza msaada wa CORDS katika shule hiyo, umesaidia wanafunzi kuendelea kusoma kwani wamepatiwa vifaa mbali mbali saidizi.


Mwenyekiti wa kijiji cha Ngoswaki,  Karia Mollel alisema jamii za kifugaji bado hazithamini sana elimu lakini, jitihada kubwa zinaendelea kufanywa na serikali na wadau wengine kuhakikisha wanatoto wanasoma na kuzuia tatizo la ndoa za utotoni.


"Ni kweli jamii yetu inachangamoto kubwa katika kuhakikisha watoto wanasoma, ila tunajitahidi kuwabana wazazi wanaozuia watoto kwenda shule lakini pia tunahamasisha chakula kupelekwa shuleni ili watoto wasome vizuri"alisema


Meneja Elimu wa Shirika la CORDS,Ezekiel Piniel alisema jukwaa hilo limeandaliwa kupitia mradi wa Kupambana na Umasikini,kupitia Elimu na Uwezeshaji wa Kiuchumi(BELIEF) ambao unadhaminiwa na  Shirika la Stromme Foundation mradi unaolenga kusaidia wanafunzi ,vikundi vya ujasiriamali na vijana wilayani Longodo na Ngorongoro.


Piniel alisema katika mradi huo,katika wilaya ya Longido, wanafunzi katika shule mbili za Ngoswaki na Longido wanasaidiwa,kupatiwa vifaa vya kujifunzia,kusaidia uboreshaji wa madarasa na mazingira ya shule,kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum,.


"Pia katika mradi huu tunasaidia vijana katika stadi mbalimbali za maisha kupitia programu ya Bonga lakini pia tunasaidia vikundi mbali mbali vya wajasiriamali kwa kuvijengea uwezo juu ya utunzaji kumbukumbu, kusimamia miradi na kuweza kuhifadhi fedha"alisema


Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Longido, Ndugu Nestory Dagharo, akizungumzia changamoto za elimu katika wilaya hiyo, alisema suala la uchangiaji chakula katika shule ni lazima katika wilaya hiyo.


Dagharo alisema, chakula ambacho wazazi wanachanga ni kile kile ambacho wangewapa wanafunzi, majumbani kwao hivyo hakuna sababu za wazazi kutochangia chakula shuleni.


Akizungumzia uandikishaji watoto na Utoro, alisema halmashauri hiyo, inafanya vizuri kwani kila mwaka inaongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa  na pia suala la utoro na ndoa za utotoni vinaendelea kudhibitiwa katika wilaya hiyo.


MWISHO

No comments: