Na Mwandishi wetu, ARUSHA
maipacarusha20@gmail.com
Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Shirikisho la Russia, Maksim Reshetnikov, amesema Russia iko tayari kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania kupitia uwekezaji katika sekta za kilimo, nishati, viwanda, usafirishaji na utalii.
Akizungumza katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Russia lililofanyika jijini Arusha, Reshetnikov alisema kampuni za Russia ziko tayari kuwekeza katika uzalishaji, usindikaji na ufungashaji wa mazao mbalimbali ya kilimo nchini Tanzania.
Alisema Russia ipo tayari kuongeza uagizaji wa kahawa, chai, tumbaku, karanga, matunda na mboga kutoka Tanzania sambamba na kushirikiana katika kuongeza thamani ya mazao hayo.
“Makampuni yetu yako tayari kuwekeza katika sekta hizi,” alisema Reshetnikov.
Aidha alisema Russia iko tayari kusambaza mbolea, teknolojia za kuongeza rutuba ya udongo, dawa za mifugo pamoja na kushirikiana katika programu za mbegu na ufugaji bora ili kuongeza uzalishaji wa kilimo nchini Tanzania.
USHIRIKIANO WA NISHATI
Katika sekta ya nishati, Reshetnikov alisema ukuaji wa uchumi wa Tanzania unahitaji kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme na matumizi ya rasilimali za nishati, hali inayofungua fursa kwa ushirikiano mkubwa zaidi.
Alisema kampuni za Russia zina nia ya kushiriki katika miradi ya gesi asilia nchini Tanzania kupitia uwekezaji, uhandisi na utoaji wa teknolojia za uchimbaji, usafirishaji na usindikaji wa gesi.
Pia alitaja mradi wa urani wa Mkuju River kuwa moja ya miradi mikubwa ya ushirikiano wa nishati kati ya Tanzania na Russia, huku maandalizi ya uzalishaji mkubwa yakiendelea.
NDEGE ZA MOJA KWA MOJA
Katika hatua inayotarajiwa kuongeza biashara na utalii, Waziri huyo alisema Russia na Tanzania zinaendelea na mazungumzo ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya mataifa
hayo mawili.
Alisema mazungumzo hayo yanaendelea vizuri na yanatarajiwa kukamilika katika miezi ijayo.
Kwa mujibu wake, hatua hiyo itaongeza idadi ya watalii wa Russia wanaotembelea Tanzania pamoja na kuimarisha biashara kati ya nchi hizo.
“Mwaka jana idadi ya watalii kutoka Russia iliongezeka kwa asilimia 40, lakini bado watalii 17,000 hawaonyeshi ukubwa wa fursa ya utalii iliyopo Tanzania,” alisema.
Kwenye sekta ya BANDARI, USAFIRISHAJI NA VIWANDA
Reshetnikov alisema maendeleo ya biashara hayawezi kufikiwa bila kuimarisha mifumo ya usafirishaji na hivyo Russia ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya bandari pamoja na kuanzisha njia za moja kwa moja za makontena.
Alisema Russia pia iko tayari kushirikiana katika teknolojia za kisasa za usafirishaji, mifumo ya usalama barabarani na maboresho ya miundombinu ya logistics.
Katika sekta ya viwanda, alisema Tanzania inatarajiwa kuanza uzalishaji wa vifaa vya rapid test kabla ya mwisho wa mwaka huu, akieleza kuwa huo ni mfano wa ushirikiano wa viwanda unaotarajiwa kuongezeka.
MAZUNGUMZO YA ULINZI WA UWEKEZAJI
Waziri huyo aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kusema mazungumzo yanaendelea kuhusu makubaliano ya kulinda na kuhamasisha uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Alisema makubaliano hayo yatasaidia kujenga mazingira salama kwa wawekezaji na kuleta manufaa ya muda mrefu kwa wananchi wa mataifa yote mawili.
Katika hitimisho lake, Reshetnikov alimshukuru Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, pamoja na Serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri na ushirikiano mkubwa uliooneshwa wakati wa kongamano hilo.


No comments:
Post a Comment