ARUSHA DC YAJIPANGA KUPAA KIUCHUMI KUPITIA MIRADI MIKUBWA YA UWEKEZAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 29 June 2026

ARUSHA DC YAJIPANGA KUPAA KIUCHUMI KUPITIA MIRADI MIKUBWA YA UWEKEZAJI

 

Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Arusha Dc Seleman Msumi

Na Mwandishi wetu, Arusha 


maipacarusha20@gmail.com


Halmashauri ya Wilaya ya Arusha imeendelea kuweka mikakati ya kuimarisha uchumi wake kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa apartment za kisasa, hoteli ya kitalii pamoja na soko la kisasa litakaloboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Seleman Msumi, amesema miradi hiyo inalenga kuifanya Arusha DC kuwa kitovu cha uwekezaji na kuongeza mapato ya halmashauri sambamba na kuboresha huduma kwa wananchi.


Amesema ujenzi wa apartment unatarajiwa kuongeza fursa za makazi ya kisasa kwa wakazi na wageni wanaofika wilayani humo, huku ukiwa chanzo cha mapato kupitia kodi na huduma mbalimbali.


Kwa mujibu wa Msumi, hoteli ya kitalii itasaidia kuongeza uwezo wa halmashauri kupokea watalii na wawekezaji wanaotembelea Arusha, mkoa unaotambulika kimataifa kwa utalii.


Ameeleza kuwa uwepo wa hoteli hiyo utafungua ajira kwa vijana katika sekta za utalii, ukarimu na huduma nyingine zinazohusiana na biashara.


Aidha, halmashauri imepanga kujenga soko la kisasa lenye miundombinu bora litakalowapa wafanyabiashara mazingira salama na rafiki ya kufanya biashara zao.


Msumi amesema soko hilo litasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha usafi pamoja na kupanua fursa za biashara kwa wananchi wa Arusha DC na maeneo jirani.


Ameongeza kuwa miradi hiyo inaendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia uwekezaji, biashara na maendeleo ya miundombinu.


Wananchi wametakiwa kuendelea kushirikiana na halmashauri katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa kizazi cha sasa na kijacho

No comments: