. *_Asema Karatu ni kitovu cha utalii kwa kuwa na hoteli za hadhi ya kimataifa_*
. *_Asema Rais Samia amedhamiria kuweka taa za barabarani na kujenga barabara za kuingia hotelini_*
. *_Ataka Uongozi wa Karatu kulinda vivutio na usafi Mji wa Karatu_*
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla ameutaka Uongozi wa Wilaya ya Karatu kuweka mkakati wa kukuza utalii katika Wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatunza mazingira na kulinda hifadhi za utalii zilizopo katika Wilaya hiyo.
Mhe. Makalla amebainisha hayo leo Jumatatu Juni 29, 2026 wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Karatu kilichokuwa kikijadili hoja za mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali, akiitaja Karatu kama nguzo kuu ya Utalii kwa Mkoa wa Arusha kutokana na kuwa lango la kuingia kwenye hifadhi za Ngorongoro pamoja na Serengeti.
"Nimekuja kuwakumbusha dhamana mliyonayo katika kuchochea utalii. Je Wilaya hii au Halmashauri hii itaendelea kuwa hivi kwa mazingira haya wakati ni kitovu cha utalii? Niwatake Wilaya hii na ninyi Waheshimiwa Madiwani wekeni mkakati wa kuboresha utalii naa kuliangalia suala la usafi wa mazingira ya Karatu." Amesema Mhe. Makalla.
Mhe. Makalla amezungumzia pia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na kuweka taa za barabarani kutokea Mto wa Mbu hadi kwenye lango la hifadhi ya Ngorongoro, ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Kilomita 10 kuingia kwenye hoteli za Karatu pamoja na kujenga barabara ya tabaka gumu kwenda Serengeti, akitaka Uongozi wa Karatu kuhakikisha wanazingatia usafi wa mazingira kuendana na uwekezaji huo mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Bw. Juma Hokorororo na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Engelbert Aloyce Qorro wameahidi kufanyia kazi maelekezo ya Mhe. Makalla, wakisisitiza pia kuendelea kukusanya mapato kwa wingi pamoja na kuandaa mkakati wa ukuzaji utalii ili pia kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na utalii.


No comments:
Post a Comment