Na Prisca Libaga Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini DCEA, Aretas James Lyimo, amesema Tanzania inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzuia na kutokomeza biashara na matumizi ya dawa za kulevya, sambamba na kuwajengea waraibu ujuzi kupitia mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA ili kuwasaidia kuepuka kurejea kwenye matumizi ya dawa hizo.
Amesema hayo jijini Arusha katika jukwaa lililowakutanisha zaidi ya vijana 200 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na mataifa mengine, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu za kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya.
Jukwaa hilo limejadili mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kinga, tiba na urekebishaji wa waathirika, hususan vijana.
Baadhi ya vijana walioshiriki, akiwemo Deogratias Ramale kutoka Tanzania na Mofolo Bisika kutoka Malawi, wameeleza umuhimu wa elimu hiyo katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya na kusaidia urejeaji wa kijamii kwa waraibu.
Wadau wa maendeleo walioshirikiana kuandaa jukwaa hilo, akiwemo Hawa Omar kutoka Tanzania na George Ochieng kutoka Kenya, wamesisitiza kuwa ushiriki wa vijana ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, huku wakitaka serikali kuimarisha programu za kinga na urekebishaji katika ngazi ya jamii.



No comments:
Post a Comment