Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imezindua jengo jipya la Ofisi ya Mkoa wa Morogoro lililogharimu Shilingi bilioni 1.63.
Katika uzinduzi huo imesisitizwa umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa tija na mianya ya rushwa inazuiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, alisema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika ujenzi wa ofisi za taasisi hiyo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Alisema Serikali imeendelea kuiwezesha TAKUKURU kwa rasilimali watu, vitendea kazi na fedha za kujenga miundombinu ya kisasa, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Kwa idadi ya majengo yanayojengwa na yaliyokwishajengwa, ni wazi kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kuimarisha taasisi hii. Huu ni ushahidi wa dhamira yake ya kuendelea kupambana na rushwa nchini,” alisema Chalamila.
Aidha Chalamila alibainisha kuwa TAKUKURU ina jumla ya ofisi 145 nchini, zikiwemo ofisi za mikoa 28, wilaya 111 na vituo maalumu sita. Hata hivyo, kati ya hizo, ni ofisi 70 pekee zinazomilikiwa na taasisi hiyo, huku ofisi 64 zikiendelea kutumia majengo yasiyomilikiwa na TAKUKURU.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa TAKUKURU, katika mwaka wa fedha 2025/2026 taasisi hiyo inaendelea kujenga majengo 11 mapya, likiwemo jengo moja la mkoa na majengo 10 ya wilaya.
“Morogoro ni miongoni mwa mikoa iliyobahatika kufikiwa mapema katika mpango huu wa ujenzi wa majengo ya kudumu ya TAKUKURU,” alisema.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Usimamizi wa Milki wa TAKUKURU, Dkt. Emmanuel Kiyabo, alisema mradi huo ulitekelezwa kwa gharama ya Shilingi 1,627,857,615.81, ikiwa ni ongezeko la Shilingi milioni 27.8 kutoka bajeti ya awali ya Shilingi bilioni 1.6.
Alieleza kuwa ongezeko hilo la asilimia 1.74 lilitokana na maboresho ya kiufundi yaliyofanyika wakati wa utekelezaji wa mradi, ikiwemo kuongeza mota za kufungua na kufunga mageti yote mawili ya uzio, kuongeza eneo la paving blocks na kazi za kuboresha eneo la kuingilia kutoka barabarani.
Dk Kiyabo alisema mradi ulianza Machi 6, 2025 na ulitarajiwa kukamilika Januari 5, 2026, lakini ulikamilika Machi 30, 2026 baada ya kuchelewa kwa takribani miezi mitatu.
Alitaja sababu za kuchelewa kwa mradi kuwa ni uhaba wa mabati ya kuezekea, kuchelewa kupatikana kwa vifaa vya ukuta wa vioo, mvua za masika pamoja na kusitishwa kwa baadhi ya shughuli kufuatia mazingira yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mradi huo ulitekelezwa kwa mfumo wa Design and Build kupitia ushirikiano kati ya TAKUKURU na Shirika la Magereza (PCS), ambapo wataalamu kutoka taasisi hizo walihusika katika usanifu, usimamizi na utekelezaji wa kazi za ujenzi.
Jengo hilo limejengwa katika eneo la Kihonda Kilimanjaro, Manispaa ya Morogoro na linajumuisha jengo kuu la ofisi lenye ghorofa moja, nyumba ya walinzi, nyumba ya jenereta na miundombinu mingine ikiwemo tenki la maji la lita 60,000, mnara wa matenki ya maji, uzio wa kisasa pamoja na eneo la maegesho na bustani.
Katika hotuba yake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU pia akawataka watumishi wa taasisi hiyo kuyatunza majengo mapya yanayojengwa na Serikali ili yaweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na TAKUKURU katika kusimamia matumizi ya fedha za umma zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Alisema halmashauri zinapaswa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za miradi inayotekelezwa pamoja na fedha zinazotumika ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.
“Ni muhimu wananchi wakafahamu miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kushiriki kuifuatilia. Hii itasaidia kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na kuzuia mianya ya rushwa,” alisema.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu dhidi ya rushwa kwa vijana kupitia Klabu za Wapinga Rushwa shuleni, akieleza kuwa kujenga kizazi kinachochukia rushwa ni msingi muhimu wa mafanikio ya mapambano hayo kwa siku zijazo.
Uzinduzi wa jengo hilo ulihudhuriwa na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, Kamati ya Usalama ya Mkoa, watumishi wa TAKUKURU, wanafunzi wa Klabu za Wapinga Rushwa pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment