Na Mwandishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
MADINI ya Tanzanite ya thamani ya zaidi ya shilingi milioni 993 yameuzwa kwenye minada miwili iliyofanyika hivi karibuni katika jengo la Tanzanite Exchange Centre mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Afisa madini mkazi Mirerani (RMO) George Kaseza, ameyasema hayo kwenye ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Kenani Laban Kihongosi alipotembelea jengo hilo na kukagua akiwa ameongozana na viongozi wa mkoa na wilaya.
Kaseza amesema minada miwili ilifanyika hivi karibuni ambapo mnada wa kwanza wa mabroka ulifanyika Mei 15 mwaka 2026 kwa washiriki 84 na madini ya shilingi 271,270,100 yalinunuliwa.
"Mnada wa pili wa dealers ulifanyika Mei 21 mwaka 2026 na madini ya thamani ya shilingi 721,750,000 yalinunuliwa," amesema RMO Kaseza.
Amesema jengo la Tanzanite Exchange Centre linamilikiwa na Halamshauri ya Wilaya ya Simanjiro ila linaendeshwa na Tume ya Madini kupitia ofisi yake.
Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo Kenani Laban Kilongosi amewapongeza watumishi wa ofisi ya RMO Mirerani kwa namna wanavyofanya kazi katika eneo hilo.
Kenani amesema tayari soko hilo limeanza kuonyesha matokeo chanya ya uwekezaji huo kutokana na mwitikio mkubwa wa wafanyabiashara na mafanikio ya minada iliyofanyika ndani ya muda mfupi tangu kuanza kutumika.
MWISHO


No comments:
Post a Comment