Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
NAIBU Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Maulid Mwatawala, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza uwekezaji katika tafiti, ubunifu na teknolojia za uzalishaji wa mbegu bora ili kuongeza tija ya kilimo na kuimarisha usalama wa chakula nchini
Ameitoa kauli hiyo wakati wa mjadala wa masuala ya uwekezaji katika miradi ya maendeleo ya uzalishaji wa mbegu na ubunifu wa teknolojia za kilimo ulioandaliwa na SUA kwa kushirikisha wadau wa sekta ya kilimo, wakiwemo watafiti, taasisi za kifedha, wazalishaji wa mbegu na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
Prof.Mwatawala alizungumza hayo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa SUA, ambapo alisema maendeleo ya sekta ya kilimo yanategemea kwa kiwango kikubwa uwekezaji katika teknolojia rahisi, tafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.
Alisema matumizi ya teknoloji na mbegu bora yanaweza kuongeza uzalishaji wa mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na kuwasaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Alisisitiza haja ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, Serikali na sekta binafsi.
Prof. Mwatawala alieleza kuwa SUA itaendelea kutoa mchango wake katika kuzalisha maarifa, teknolojia na wataalamu watakaosaidia kuendeleza sekta ya kilimo na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wakulima kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, alisema taasisi hiyo imejipanga kuimarisha ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji wa mbegu ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zilizothibitishwa na zenye ubora unaotakiwa.
Chimagu alisema uuzaji wa mbegu feki unahatarisha mafanikio ya wakulima na unaweza kusababisha hasara kubwa katika uzalishaji wa mazao, jambo linaloweza kuathiri juhudi za taifa katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha.
“Hatutasita kuchukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayebainika kukiuka sheria za uzalishaji na uuzaji wa mbegu.Tunataka kulinda maslahi ya wakulima na kuhakikisha wanapata mbegu bora zinazowezesha kuongeza uzalishaji,”alisema Chimagu.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Mkani Waziri, alisema kuna umuhimu wa mifumo ya sekta ya kilimo kuunganishwa kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima.
Alisema matumizi ya mifumo ya kidijitali yatawawezesha wakulima kupata mikopo na huduma nyingine za kifedha kwa urahisi zaidi bila kujali mahali walipo, hatua itakayochochea ukuaji wa sekta ya kilimo na kuongeza ushiriki wa wakulima katika uchumi wa kisasa.
Wadau waliohudhuria mjadala huo walikubaliana kuwa uwekezaji katika mbegu bora, teknolojia za kisasa, tafiti za kilimo na huduma za kifedha ni nguzo muhimu katika kuifanya sekta ya kilimo kuwa yenye tija, ushindani na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
.......



No comments:
Post a Comment