Rais Samia ataka fursa zaidi ufadhili wa masomo - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 4 June 2026

Rais Samia ataka fursa zaidi ufadhili wa masomo

 


Mwandishi Wetu, MOSCOW

 

maipacarusha20@gmail.com 


RAIS Samia Suluhu Hassan amesifu mchango wa Serikali ya Urusi kwenye maendeleo ya Tanzania kupitia ufadhili wa masomo na kusema ufadhili huo ni muhimu kwa ukuaji wa taifa.

 

Akizungumza jijini Moscow, Urusi mara baada ya kupokea Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha RUDN nchini humo, Rais Samia alisema wakati taifa hilo la kigeni likiendelea kutoa mchango huo, serikali yake nayo imeongeza ufadhili kwa wanafunzi wenye uhitaji.

 

Rais Samia alisema RUDN imetoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi zaidi ya 1100 kutoka Tanzania, huku wanafunzi wengine zaidi ya 5,000 wakipata ufadhili kupitia mpango wa Samia Scholarship ulioanzishwa baada ya yeye kuingia madarakani.

 

“ Elimu imethibitika kuwa ndiyo njia pekee ya kubadilisha maisha ya watu. Safari ya mtu kutoka kuwa hajui chochote na masikini na kusoma kufikia kuwa daktari, mwanasayansi au mwalimu ni mojawapo ya safari za kusisimua za maisha ya mwanadamu.

 

“ Tunaipongeza na kuishukuru serikali ya Urusi kwa mchango wake kwenye sekta ya elimu lakini tutafurahi kama ufadhili utaongezeka. Kwa upande wetu, tutaendelea kufadhili wanafunzi wenye uhitaji,” alisema.

 

RUDN imekuwa na mahusiano ya muda mrefu na Tanzania, kikiwa kimesomesha zaidi ya Watanzania 1,100 tangu kianzishwe mwaka 1960  iliyopita na sasa wanafunzi wa Kitanzania 72 wanapata mafunzo katika ngazi mbalimbali chuoni hapo.

 

Rais Samia anakuwa Rais wa karibuni zaidi kupewa heshima hiyo na chuo hicho, huku marais wengine sita wakiwa wamewahi kupewa tuzo hiyo. Baadhi ya marais hao ni Sam Nujoma wa Namibia, Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Olesegun Obasanjo wa Nigeria.

 

Vyuo vikuu vingine saba ambavyo vimewahi kumtunukia Rais Samia shahada za namna hiyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Jawahral Nehru nchini India, Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki, Nasarawa nchini Nigeria, Chuo Kikuu cha Anga cha Korea Kusini, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).

 

Rais Samia yuko nchini Urusi katika ziara ya kitaifa iliyoanza jana na itahitimishwa kesho baada ya kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi wa St. Petersburg nchini hapa.

No comments: