![]() |
| MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga |
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewataka madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kuchangamkia fursa ya miradi ya hewa ya ukaa ili jamii iweze kunufaika kwa maendeleo.
RC Sendiga ameeleza hayo mji mdogo wa Orkesumet, kwenye kikao cha baraza la madiwani, ambapo alizindua basi lililonunuliwa kupitia fedha za mapato ya ndani, kuzindua samani mpya za ukumbi na kupokea taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ya mwaka 2024/2025 ambapo Simanjiro imepata hati safi.
Amesema endapo madiwani wa Simanjiro wakiridhia mradi wa utunzaji mazingira wa hewa ukaa wataweza kunufaika kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Wenzenu wa wilaya ya Kiteto wamefaidika mno na miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kupitia utunzaji wa hewa ukaa hivyo nanyi mnapaswa kuchangamka," amesema RC Sendiga
Amewatoa hofu madiwani hao juu ya kuwa na wasiwasi na miradi ya hewa ukaa kwani ina tija kwa jamii kupitia miradi ya maendeleo na pia utunzaji wa mazingira katika eneo hilo.
"Simanjiro sasa na ninyi changamkieni fursa hii ya miradi ya hewa ukaa ili mnufaike na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule na mingineyo ambayo inapatikana," amesema RC Sendiga.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Kaleya Mollel amesema wamepokea maelekezo hayo na watayafanyia kazi miradi ya hewa ya ukaa.
Mollel amesema miradi ya hewa ya ukaa inatunza mazingira na pia inafanikisha maendeleo hivyo watahakikisha wanafanikisha ili ianze rasmi.
Mmoja kati ya wakazi wa wilaya ya Simanjiro, Esupati John amesema miradi wa hewa ya ukaa ni mzuri kwani unatunza mazingira na fedha za maendeleo zinapatikana.
Esupati amesema baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanahofu na uwekezaji huo ila wanapaswa kukubaliana nao kwani hauna madhara na pia unahifadhi mazingira.
Mkazi mwingine Aloyce Balthazar amesema maeneo ya jamii ya wafugaji wa Kiteto na Longido mkoani Arusha wamefaidika na miradi ya hewa ya ukaa hivyo iungwe mkono.
Amesema baadhi ya watu wanahofia miradi ya hewa ya ukaa wakidhani watanyimwa kuchunga mifugo katika maeneo hayo suala ambalo siyo la kweli.
MWISHO



No comments:
Post a Comment