![]() |
Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Kutokana na uwepo wa tishio la ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuratibu na kuimarisha mifumo ya utayari kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya dharura na milipuko inayoweza kuingia nchini.
Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Maafa, Dk. Erasto Sylvanus, alisema hayo wakati wa mafunzo ya wataalamu wa matibabu ya magonjwa ya dharura na milipuko (EMT) kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Dk. Sylvanus alisema serikali imejitahidi kuimarisha mifumo ya utayari wa kukabiliana na magonjwa ya dharura na milipuko. Alieleza kuwa kupitia mifumo hiyo, inawezekana kutambua magonjwa ya dharura yanayoweza kutokea, wakati yanapoweza kutokea na namna bora ya kuyakabili.
"Ikitokea ugonjwa wowote wa dharura au mlipuko, tunajua kabisa kuwa tunayo timu ya kudumu ya kukabiliana nao. Timu hii imejengewa uwezo wa kufanya kazi popote, iwe ndani au nje ya nchi. Pia imehusisha wataalamu wa afya kutoka Tanzania Bara na Zanzibar," alisema Dk. Sylvanus.
Aliiitaka timu hiyo kutumia ujuzi na maarifa waliopata kuimarisha uwezo wa taasisi wanazotoka ili kuwa na timu za dharura kwenye taasisi hizo. Pia aliwasisitiza kuendelea kuzingatia viwango vya kimataifa ili kuwa na timu inayotambulika kikanda na kimataifa, itakayoweza kufanya kazi ndani na nje ya nchi.
Aidha, aliwataka kufanya kazi kwa ushirikiano bila kujali taasisi wanazotoka, kuwa wazalendo kwa kuwa tayari kufanya kazi wakati wowote na mahali popote kwa haraka, kuimarisha kanzidata ya timu hiyo, pamoja na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuendeleza ujuzi walioupata.
Kwa upande wake, Afisa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Janeth Masuma, alisema Tanzania ipo tayari kukabiliana na Ebola pamoja na magonjwa mengine ya dharura na milipuko, kutokana na kuwa na timu ya wataalamu wenye uwezo na utayari wa kutoa huduma wakati wowote.
Alieleza kuwa endapo majanga yoyote ya kiafya yatatokea, timu hiyo itakuwa mstari wa mbele katika kuyakabili kwa haraka, hali itakayosaidia kupunguza vifo.
"Tanzania ni nchi ya 27 barani Afrika kuanzisha timu ya kitaifa ya kukabiliana na magonjwa ya dharura na milipuko. Kwa sasa, timu hii ipo imara na tayari kukabiliana na magonjwa yoyote ya dharura," alisema Dk. Masuma.
Naye Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Kitengo cha Dharura na Maafa cha Wizara ya Afya, Dk. Erick Richard, alisema mafunzo hayo yalianza mwaka jana kufuatia utaratibu uliowekwa na WHO katika utoaji wa huduma za dharura.
Alisema timu hiyo haitakuwa ya kitaifa pekee, bali inaweza kutumika hata nje ya nchi endapo itahitajika.
Dk. Richard aliongeza kuwa, mbali na kutoa huduma za matibabu wakati wa magonjwa ya dharura na milipuko, timu hiyo itasaidia pia kuimarisha timu za dharura katika taasisi za afya wanazotoka.
Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Dk. Hussein Manji, alisema timu hiyo ya kitaifa inajumuisha wataalamu kutoka hospitali za serikali na binafsi, wakiwemo wauguzi, madaktari na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya afya.
"Kama nchi, sasa tunayo timu ya kukabiliana na magonjwa ya dharura na milipuko yenye jukumu la kudhibiti na kutoa matibabu. Timu hii inaundwa na wataalamu wa afya kutoka sekta mbalimbali zinazohusika na huduma za afya," alisema Dk. Manji.
Dk. Manji aliishukuru Wizara ya Afya kwa kushirikiana na WHO kuandaa mafunzo hayo, yaliyowezesha kupatikana kwa timu yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya dharura na milipuko wakati wowote, na hivyo kuhakikisha Watanzania wanabaki salama.
Mwisho..


No comments:
Post a Comment