Burhani Yakub, Handeni.
maipacarusha20@gmail.com
Wafanyabiashara wa Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga wamehimizwa kulipa kodi bila kushurutishwa kwa kuwa fedha hizo ndizo zinazotumika kuendesha shughuli za maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni,Salum Nyamwese ametoa agizo hilo leo wakati wa uzinduzi wa kituo cha huduma cha Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkata kilichopo Mkata Wilayani hapa.
Amesema kutokana na TRA kuweka mazingira rafiki ya ulipaji wa kodi hakuna sababu ya baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi mbalimbali walizokadiriwa kwani zinatumika kuendeshea shughuli za maendeleo.
"Wananchi na wafanyabiashara tuepuke kukwepa kulipa kodi mbalimbali tulizokadiriwa kwa kuwa fedha hizo ndizo zinazotumika kuendesha shughuli za maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu,maji na huduma mbalimbali za kijamii"amesema Nyamwese.
Akizungumzia kuhusu kituo cha huduma kodi cha Mkata,Mkuu huyo wa Wilaya amesema kimewekwa wakati sahihi Kwa kuwa eneo hilo kwa sasa ni la kimkakati wa kiuchumi,usafirishaji na huduma za kijamii.
"Mkata ni eneo linalopitiwa barabara inayounganisha si Mikoa mbalimbali pekee bali na nchi za Afrika Mashariki na Maziwa makuu...ni eneo ambalo biashara inakua kila kukicha na mzunguko wa fedha unaongezeka"amesema Nyamwese.
Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, CPA,Castro John amesema kituo cha huduma za kodi Mkata kitatoa huduma za utatuzi wa changamoto zunazowakabili wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa Mkata,Kabuku,Segera na maeneo ya jirani kwa wakati na haraka kuliko ilivyo kuwa awali ambapo walikuwa wakilazimika kuzifuata Handeni mjini.
Huduma nyingine ni ukadiriaji wa mapato utoaji wa TIN namba pamoja na uwezeshaji wa biashara kwa wafanyabiashara wadogo.
"Jengo hili ni la kisasa ni ofisi yenye kuvutia kuliko hata baadhi ya ofisi za TRA Wilaya lakini tumepanga,ombi letu kwako Mkuu wa Wilaya ni kupewa kiwanja ili tuweze kujenga ofisi yetu kubwa na yenye hadhi ya TRA"amesema CPA Castro.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni,Musa Mwanyumbu amesema kuzinduliwa kwa kituo cha TRA Mkata ni faraja kwa wafanyabiashara wa eneo hilo ambao walikuwa wakilazimika kupoteza muda na fedha kufuata huduma za kikosi mjini Handeni.
"Tumepata faraja kubwa kwani hili lilikuwa ombi letu la muda mrefu tukiomba kuletewa ofisi Mkata...ilikuwa wafanyabiashara wakitaka kulipa kodi lazima wasafiri kwenda Handeni na huko wanapoteza siku nzima au siku mbili"amesema Mwanyumbu.
Katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara wadogo JWT Mkoa wa Tanga Ismail Masoud amewataka wajasiliamali kujitokeza TRA Mkata ili wajiandikishe kwa ajili ya kutambulika.
"Wajasiliamali jitokezeniTRA mkapate TIN namba hii itawasaidia kutambulika na kuraaimishwa kwa biashara zenu ndogo ndogo"amesema Ismail.
MWISHO

No comments:
Post a Comment