WAKULIMA SINGIDA WAIBUA HOJA MAFAO YA UZEENI ‎ - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 7 June 2026

WAKULIMA SINGIDA WAIBUA HOJA MAFAO YA UZEENI ‎

 

Mkuu wa mkoa Sgd Halima Dendego akipokea zawadi ya picha ya pamba.


Maandamano ya Jukwaa la vyma vya ushirika yaliyoanzia kituo cha afya sokoine kwenda ukumbi wa luluma na kupokewa na mkuu mkoa.

Baadhi ya washiriki wa jukwaa la maendeleo vyama vya ushirika mkoa Singida

‎Na Seif Takaza, Singida


‎maipacarusha20@gmail.com

‎Hofu ya maisha baada ya uzee imeibua wito mpya kutoka kwa wakulima, ambao sasa wanaishinikiza Serikali ianze kuwaingiza kwenye mifumo ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ili nao waanze kunufaika na mafao ya uzeeni,na hivyo kutoa nafuu, na kuwa na uhakika wa maisha bora watakapostaafu shughuli za kilimo.

‎Ombi hilo limetolewa na viongozi wa vyama vya msingi vya kilimo (Amcos), kwenye mkutano wa Jukwaa la Maendeleo ya Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, lililofanyika mkoani Singida.

‎Mmoja wa washiriki, Athumani Iddi, kutoka Umoja Amcos Kata ya Mtoa, Tarafa ya Shelui, Wilaya ya Iramba, alisema kwa kuwa wakulima hutegemea pato kutokana na mazao yao, ni vyema sasa waanze kuandaliwa na kuingizwa kwenye mfumo rasmi wa akiba, tayari kwa ajili ya kumudu maisha yao ya baadaye.

‎Kutokana na hali hiyo, Iddi ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu mzuri wa kukata sehemu ya mapato yao ya mauzo ya mazao kupitia vyama vya msingi, na kuyapeleka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, kwa ajili ya pensheni, baada ya kustaafu kilimo.

‎Alitolea mfano kwa watumishi wa umma na baadhi ya wafanyakazi wa sekta binafsi, ambao hunufaika na mafao baada ya kustaafu kutokana na michango yao wakati wa ajira, hivyo wakulima nao wanastahili kuwekewa mfumo huo rafiki unaofanana, ili baadaye wapate kinga ya kiuchumi wakati wanapozeeka.

‎Akijibu hoja hiyo katika jukwaa Hilo, Afisa Ushirika wa Wilaya ya Manyoni, Christopher Lyamuganda, alisema kuwa utekelezaji wa pendekezo hilo unahitaji mchakato mpana kisheria, unaohusisha pia maandalizi ya sera na sheria za nchi zitakazowasilishwa na kujadiliwa kwa kina na Bunge, kabla ya kuanza kutumika rasmi.

‎Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Ushirika Mkoa Singida, Nuria Gulamali, alivitaka vyama vya msingi vya ushirika, kuhakikisha vinafungua na kutumia akaunti za benki katika shughuli za kifedha ili kuimarisha uwazi na kuondoa mianya ya ubadhirifu wa fedha za wakulima.

‎Gulamali pia alipiga marufuku vyama vya ushirika kupokea fedha taslimu kutoka kwa makampuni yanayojishughulika na ununuzi wa mazao, na kusisitiza malipo yote yanapaswa kufanyika kupitia akaunri za benki, ambao ndio mfumo rasmi, na maelekezo ya Serikali.

‎Alisema viongozi wa vyama hawapaswi kupokea fedha za vyama kupitia simu zao binafsi, na pia wakulima wasiokuwa na akaunti, wahakikishe wanakuwa nazo, ili kurahisisha malipo na kuongeza usalama wa fedha. Kaulimbiu ya ushirika mwaka 2026 ni, “Ushirika kwa Dunia Yenye Amani, Linda Ushirika Chagua Uadilifu.”


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Singida Daudi Ngayaula, aliwaomba wakulima,viongozi na jamii kwa ujumla, kudumisha upendo, ili Taifa liendelee kuwa na amani katika kuihakikishia jamii kushiriki shughuli za maendeleo bila hofu wala usumbufu.


Alibainisha kuwa uwepo wa migogoro na kukosekana kwa hali ya amani, kunaweza kudhoofisha juhudi za jamii na wakulima, na hivyo kuathiri juhudi na mafanikio ya vyama vya ushirika.


‎Ngayaula alisema kuwa usitawi wa vyama vya ushirika unategemea zaidi uwepo wa hali ya amani na utulivu, hivyo changamoto ya migogoro inapaswa kishibitiwa ili ikose nafasi ya kudhoofisha juhudi za wakulima katika kuelekea mafanikio yao.


‎MWISHO

No comments: