Walimu 141 wa Meru watunukiwa tuzo, halmashauri yalenga ufaulu wa asilimia 100 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 29 June 2026

Walimu 141 wa Meru watunukiwa tuzo, halmashauri yalenga ufaulu wa asilimia 100

 


 Na Mwandishi wetu, MERU


maipacarusha20@gmail.com 


Halmashauri ya Wilaya ya Meru imewakabidhi tuzo walimu 141 pamoja na makombe kwa walimu waliofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili, kidato cha nne na kidato cha sita kwa mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kuboresha sekta ya elimu.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Lucas Kaaya, alisema walimu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya elimu na mafanikio ya wanafunzi, hivyo wanapaswa kuthaminiwa na kupewa motisha ya kutosha.


Kaaya alisema uongozi wa halmashauri unatambua mchango mkubwa wa walimu na uko tayari kushughulikia changamoto zinazowakabili ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Alisema miongoni mwa masuala atakayoyasimamia ni madai ya walimu pamoja na kuhakikisha wanapata motisha pale inapohitajika, akieleza kuwa ustawi wa walimu una mchango mkubwa katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Mwalimu Zainabu Mwakinya, alisema walimu wa halmashauri hiyo wameendelea kuiletea heshima Meru kupitia matokeo mazuri ya mitihani ya taifa.

Alisema kutokana na juhudi hizo, halmashauri imefanikiwa kupata makombe mengi katika ngazi ya taifa, jambo linalodhihirisha ubora wa ufundishaji unaotolewa shuleni.

Naye Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Meru  Mwalimu  Marcel Itambu alisema jumla ya walimu 141 wametunukiwa tuzo kutokana na utendaji wao bora katika matokeo ya mitihani ya mwaka 2025.


Alisema pia hali ya ufaulu imeendelea kuongezeka katika ngazi mbalimbali za elimu ya sekondari wilayani humo.


Kwa mujibu wa afisa huyo, ufaulu wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 96 mwaka uliopita hadi asilimia 98, huku kidato cha pili ukiongezeka kutoka asilimia 94 hadi asilimia 95.


Alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi, wazazi na uongozi wa halmashauri katika kuimarisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.


Aidha, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Meru imejipanga kuhakikisha mwaka 2026 wanafikia lengo la kupata ufaulu wa asilimia 100 katika mitihani ya taifa, huku akiwasisitiza walimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi.

No comments: