WALIMU WAHIMIZWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA AKILI UNDE (AI) KUBORESHA UFUNDISHAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 28 June 2026

WALIMU WAHIMIZWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA AKILI UNDE (AI) KUBORESHA UFUNDISHAJI





Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewahimiza walimu kote nchini kushiriki kikamilifu katika matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.


Mratibu wa EdTech kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Alcardo Alex, amesema serikali imeweka kipaumbele katika matumizi ya teknolojia zinazoibukia, hususan Akili Unde, ili kuimarisha sekta ya elimu.


"Wizara imeandaa miongozo ya matumizi ya teknolojia ya Akili Unde katika ngazi zote za elimu, kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu, kwa lengo la kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji," alisema Dk. Alex.


Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu wa Lugha ya Kiingereza Tanzania (TELTA), Dk. Alex alisema wizara inaendelea kuhamasisha walimu, hususan wa somo la Kiingereza, kutumia teknolojia ya AI ili kuongeza ufanisi na kuimarisha ujuzi wao wa kufundisha.


Alisema serikali tayari imekamilisha madarasa janja 210 ambayo yameanza kutumika, huku lengo likiwa ni kusambaza madarasa hayo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.


Kwa mujibu wake, matumizi ya Akili Unde yatawasaidia walimu kuandaa vipindi vya masomo, kutunga na kusahihisha mitihani, pamoja na kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa ufanisi zaidi.


"Ni muhimu walimu kujifunza na kutumia teknolojia ya Akili Unde kwani ni fursa ya kuongeza maarifa, kubadilishana uzoefu na kuboresha ubora wa elimu," alisema Dk. Alex.


Kwa upande wake, Mratibu wa TELTA, Dk. Ayoub Msuya, alisema matumizi ya AI yatawasaidia walimu kuandaa masomo kwa ubora zaidi na kuwasaidia wanafunzi kuelewa lugha ya Kiingereza kwa urahisi.


Aliongeza kuwa teknolojia hiyo pia itawasaidia walimu kutambua mbinu bora za kufundishia na kuchagua nyenzo zinazofaa zaidi wakati wa ufundishaji darasani.


Naye Mkuu wa Idara ya Taaluma za Lugha katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dk. Onesimo Nyinodi, alisema idara yake imepewa jukumu la kuratibu mafunzo ya matumizi ya Akili Unde kwa walimu wa lugha ya Kiingereza nchini.


Alisema hatua hiyo inalenga kuwawezesha walimu kutumia teknolojia hiyo kwa ufanisi katika kuboresha matokeo ya ujifunzaji.


..

No comments: