Burhani Yakub, Tanga
maipacarusha20@gmail.com
Wanafunzi sita wamefuzu kushiriki kongamano la. Afrika Mashariki la kupinga matumizi ya dawa za kulevya (East African Youth Forum on Drugs 2026) litakalofanyika Jijini Arusha baada ya kuibuka washindi katika mdahalo uliofanyika mjini hapa.
Mdahalo huo wa mwisho wa mchujo ulihudhuriwa na Naibu.Meya wa Jiji la Tanga,Halid Rashid huku majaji wakitoka Tume ya Kuzuia na Kupambana na dawa za kulevya.pamoja na wataalamu wabobezi kutoka Taasisi mbalimbali na wazazi na wanafunzi wa shule mbalimbali walikuwa watazamaji.
Waliofuzu kushiriki mdahalo huo ni James Martine wa kidato cha tatu kutoka shule ya Sekondari Tanga Ufundi,Halima.Bahati kidato cha nne (Old Tanga),Najash Ahmad kidato cha nne (Japan), Happiness Msumule kidato cha tatu (Nguvumali),Farhiya Said kidato cha nne (Nguvumali) na James Said kidato cha nne (Mkwakwani).
Mratibu wa kongamano hilo lililoendeshwa na Taasisi ya Gift of Hope kwa udhamini wa Fondation Botnar kupitia Tanga yetu chini ya mradi ujulilanao tuwazingatie vijana sio dawa za kulevya,Said Bandawe amesema kongamano hilo litakaloshirikisha wanafunzi kutoka shule mbalimbali za nchi za Afrika Mashariki litafanyika kuanzia alhamisi hadi jumamosi wiki hii Jijini Arusha.
Amesema mdahalo huo ni matokeo ya mafunzo ya namna ya kupambana na dawa za kulevya yaliyokuwa yakiendeshwa katika shule mbalimbali za Sekondari za Jiji la Tanga na kushirikisha zaidi ya wanafunzi 1000.
"Mdahalo huo ni matokeo ya mafunzo ya namna ya kupambana na dawa za kulevya yaliyokuwa yakiendeshwa katika shule mbalimbali za Sekondari chini ya mradi wa tuwazingatie vijana sio dawa za kulevya lengo likiwa ni baada ya kubaini kuwa hilo ni kundi lililo katika hatari ya kukumbwa na janga la matumizi ya dawa za kulevya"amesema Bandawe.
Akizungumza baada ya washindi hao kupatikana,Naibu Meya amewataka kuliwakilisha vyema Jiji la Tanga katika kongamano hilo la Afrika Mashariki kwa kuchukua elimu watakayoipata na warejeapo waisambaze kwa wenzao walio shuleni na mitaani.
"Katika kongamano la Afrika Mashariki ni wazi kuwa mtapata elimu na ujuzi zaidi wa namna ya kupambana na dawa za kulevya...mtakaporejea mtoe elimu hiyo kwa wenzenu waliopo shuleni na mitaa ya Jiji la Tanga.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao,Ahmad Kidege amesema katika mdahalo huo amebaini kwamba elimu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya imewafikia vijana wengi isipokuwa changamoto ipo kwenye utekelezaji.
"Nimewasikia washiriki wa mdahalo huu kuanzia mwanzo hadi mwisho nilichojifunza hapa nimebaini kwa elimu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya imewafikia vijana wengi isipokuwa changamoto ipo kwenye utekelezaji... nashauri kila mmoja katika kaya ashiriki kwa vitendo katika kukemea matumizi ya dawa za kulevya"amesema Kidege.
MWISHO

No comments:
Post a Comment