AFISA ARDHI IFAKARA AUWAWA, ALIKUWA NYUMBANI KWAKE NA FAMILIA YAKE. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 21 July 2026

AFISA ARDHI IFAKARA AUWAWA, ALIKUWA NYUMBANI KWAKE NA FAMILIA YAKE.

 




Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


AFISA Ardhi Msaidizi wa Mji Mdogo wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero Zakaria Rashid Malika(54) ameuwawa  na watu wasiojulikana baada ya kuvamia nyumba yake usiku na kumshambulia kwa silaha zenye ncha kali hadi kufariki dunia.


Kufatia mauaji hayo vilio, Simanzi vimetanda katika Wilayani humo.


Tukio hilo limetokea Julai 19, 2026 majira ya kati ya saa moja hadi mbili usiku,katika Kitongoji cha Kapolo, Kijiji cha Kikwawila, Kata ya Kibaoni,wilayani Kilombero ambapo familia, ndugu na wananchi wamekusanyika kwa majonzi makubwa wakati mwili wa marehemu ulipowasili nyumbani ili kuagwa.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mgogoro wa muda mrefu wa ardhi unahusishwa na tukio hilo, huku watu wawili wakishikiliwa kwa mahojiano.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Kikwawila, Saidina Faya, amesema tukio hilo limewasikitisha viongozi na wananchi wote kwani marehemu enzi za uhai wake alikuwa mtu mwema na mwenye ushirikiano na wengine.


Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kapolo, Musa Salahange, amesema taarifa za tukio hilo ziliwafikia kupitia Polisi Kata kabla ya viongozi kufika eneo la tukio na kwamba Marehemu enzi za uhai wake hakuwa na ugomvi na mwanakijiji yeyote.


Diwani wa Kata ya Kibaoni, Rashid Mwintuka, amesema mauaji hayo ni pigo kwa kata hiyo kutokana na mchango wa marehemu katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo utatuzi wa migogoro ya ardhi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amethibitisha tukio hilo na kusema watu wawili wanashikiliwa huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini waliohusika wote.


Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kutumia njia za kisheria kutatua migogoro ya ardhi na kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapobaini viashiria vya uhalifu.


Marehemu Zakaria Rashid Malika aliwahi kufanya kazi katika Halmashauri za Songea Mkoani Ruvuma, Malinyi na baadaye Mji Mdogo wa Ifakara Mkoani Morogoro ambapo alikuwa akitoa huduma za masuala ya ardhi. 


Ameacha mjane na watoto 10 na mwili wake baada ya kuagwa nyumbani kwake utasafirishwa Kuelekea Mkoani Iringa alikozaliwa, kwaajili ya Maziko.


Mwisho

No comments: