Timu ya madaktari bingwa wa kinywa na meno kutoa huduma Arumeru Magharibi Bure. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 21 July 2026

Timu ya madaktari bingwa wa kinywa na meno kutoa huduma Arumeru Magharibi Bure.

 



   Na Mwandishi wetu, Arusha 


maipacarusha20@gmail.com 


Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumayi, amesema ujio wa madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno kutoka Ujerumani ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya na kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo la madini ya fluoride kwenye maji, ambalo limekuwa likiathiri maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha.


Akizungumza baada ya kuwapokea madaktari hao, Dkt. Lukumayi alisema wataalamu hao wanatoka katika taasisi ya Dental Global ya nchini Ujerumani, ambayo imekubali kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utoaji wa huduma, mafunzo na tafiti kuhusu afya ya kinywa na meno.


Alieleza kuwa ushirikiano huo ulianza tangu alipokuwa akifanya kazi kama Mganga Mkuu wa Wilaya na baadaye Mganga Mkuu wa Mkoa, ambapo alijenga mahusiano ya karibu na taasisi hiyo na kuomba ije kusaidia Tanzania katika sekta ya afya ya kinywa na meno.


Dkt. Lukumayi alisema awali taasisi hiyo ilikuwa imekusudia kuwachukua madaktari 200 kutoka Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Ujerumani, lakini baada ya kutathmini hali halisi waliamua kuanzisha mradi mkubwa wa mafunzo utakaowezesha madaktari wengi zaidi kufundishwa hapa nchini na wengine kupata fursa ya kufanya kazi Ujerumani.


Alisema katika siku saba za ziara yao, madaktari hao wataanza kwa kutembelea shule mbalimbali kufanya uchunguzi wa afya ya meno kwa watoto, kutoa huduma za matibabu, kufanya tafiti na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ndani.


Mbunge huyo alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya, akieleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 53.7 zimeelekezwa katika kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno nchini.


Aidha alisema Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha pia mafunzo ya madaktari bingwa na mabobezi 16 wa afya ya kinywa na meno kupitia programu za ufadhili wa masomo, hatua ambayo imeongeza wataalamu wenye ujuzi nchini.


Kwa mujibu wa Dkt. Lukumayi, taasisi ya Dental Global imeonyesha nia ya kuwekeza zaidi Tanzania katika huduma za afya ya kinywa na meno na baada ya kumaliza shughuli zake Arumeru Magharibi itaendelea kutoa huduma katika maeneo mengine nchini.


Aliwataka wananchi kushirikiana na wataalamu hao ili kuhakikisha tafiti zitakazofanyika zinatoa picha halisi ya ukubwa wa tatizo la fluoride na kusaidia kupatikana kwa suluhisho la kudumu.


Dkt. Lukumayi alisema utafiti utakaofanywa utasaidia Serikali na wadau kupanga mikakati bora ya kupunguza athari za fluoride kwenye maji ya kunywa, tatizo ambalo limekuwa likisababisha changamoto kubwa za afya ya meno katika baadhi ya maeneo ya Arusha.


Alibainisha kuwa maeneo ya Oljoro na Sambu ni miongoni mwa yaliyoathirika zaidi, lakini Serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji safi utakaosaidia kupunguza kiwango cha fluoride kwenye maji katika maeneo hayo.


Mbunge huyo alisisitiza kuwa pamoja na mradi huo, bado kuna haja ya kuendelea kufanya tafiti na kushirikiana na wataalamu wa kimataifa ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.


Aidha aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na kuwakaribisha wageni wanaokuja kuwekeza na kushirikiana na nchi katika sekta mbalimbali za maendeleo.


Aliwashukuru pia waandishi wa habari kwa kuendelea kuhabarisha umma kuhusu shughuli za maendeleo na juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za kijamii nchini.

No comments: