Atuhumiwa kumuua Mama yake baada ya kunyimwa kwenda Birthday - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 30 July 2026

Atuhumiwa kumuua Mama yake baada ya kunyimwa kwenda Birthday


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase


Mwandishi wetu, Maipac Kibaha


maipacarusha20@gmail.com


Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Rahma Tito, (16) Mkazi wa kijiji cha Msoga,kwa tuhuma za mauaji ya mama yake mzazi Hadija Shaha (51).

Akizungumza na Waandiahi wa Habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase amesema tukio hilo lilitokea Julai 28 majira ya saa 5 usiku huko katika kijiji cha Msoga, Wilaya ya Kipolisi Chalinze.


Kamanda Morcase amesema mtuhumiwa alimuua mama yake Hadija Shaha mkazi wa Soga ambaye alikua na ulemavu wa miguu yote miwili kwa kumchoma kichwani kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni marehemu kumkataza binti yake Rahma kwenda kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa ya rafiki yake iliyokuwa inafanyika maeneo ya jirani na Hospitali ya Msoga.


Akielezea tukio hilo amesema, baada ya binti huyo kuzuiwa kwenda kwenye sherehe alianza kumshambulia mama yake kisha kumchoma na kitu chenye ncha kali kichwani.


Julai 29 majira ya saa moja asubuhi fundi ujenzi alifika nyumbani kwa Hadija Shaha kufuata mfuko wa saruji na fedha yake ya ujenzi ndipo alipogonga mlango na kufunguliwa na binti huyo wa marehemu.


Hata hivyo baada ya mlango kufunguliwa jirani huyo aligundua kuna mwili wa marehemu ukiwa umelala sakafuni ukiwa na majeraha kichwani.


Mwili wa marehemu ulipelekwa Hospitali ya Msoga ambapo ulifanyiwa uchunguzi wa daktari kisha ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.



Kamanda amesema uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa rai kwa wazazi ,Walezi, Viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kushirikiana katika malezi ya watoto ili kubaini tabia na changamoto za watoto wao kwenye makuzi ili hatua zichukuliwe mapema kabla hayajatokea madhara.


Mwisho
 

No comments: