MAENDELEO YA UWEPO WA AI HAYANA LENGONLA KUCHUKUA NAFASI ZA MWALIMU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 17 July 2026

MAENDELEO YA UWEPO WA AI HAYANA LENGONLA KUCHUKUA NAFASI ZA MWALIMU

 





NA LILIAN KASENENE, MOROGORO 


maipacarusha20@gmail.com


MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Prof. Sifuni Mchome, amesema maendeleo ya Akili Mnemba (AI) hayana lengo la kuchukua nafasi ya mwalimu, bali kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.


Aidha amesisitiza kuwa walimu na wakufunzi wanapaswa kujiandaa kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.


Prof. Mchome alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Baraza la Uongozi la Tano la Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), akieleza kuwa dunia imebadilika na taasisi za elimu ya ufundi hazina budi kubadilika ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.


Alisema AI ni nyenzo muhimu ya kuongeza ubora wa ufundishaji, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya mwalimu kwa kuwa kazi ya mwalimu inahusisha kujenga maadili, ubunifu, usimamizi wa mafunzo ya vitendo na kumlea mwanafunzi, mambo ambayo teknolojia pekee haiwezi kuyafanya.


Prof. Mchome alisema pamoja na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya watu wenye ujuzi wa kazi mbalimbali za mikono, wengi wao hawapo katika mfumo rasmi wa kutambua na kuthibitisha ujuzi wao, jambo linalowanyima fursa za ajira, mikopo na kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi.


Aliwatolea mfano wachongaji wa vinyago, mafundi vyuma, seremala na mafundi wengine wanaofanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika jamii, lakini hawana vyeti vinavyothibitisha uwezo wao.


"Changamoto si kwamba hatuna watu wenye ujuzi, bali wengi hawajatambulika rasmi. Tunahitaji mfumo unaowawezesha kuthibitisha ujuzi wao na kuwa sehemu ya nguvu kazi inayotambulika," alisema.


Prof. Mchome alieleza kuwa mfumo wa VET umeanza tangu miaka mingi iliyopita na kwa sasa una zaidi ya vituo 900 vya mafunzo ya ufundi nchini.


Alisema kadri mfumo ulivyokuwa unapanuka, ilionekana wazi kuwa taifa lilihitaji wakufunzi wengi zaidi wenye uwezo wa kutoa mafunzo bora, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC).


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema mamlaka hiyo inaendelea kufanya maboresho ya mafunzo ya ufundi ili yaendane na mahitaji ya uchumi wa kisasa na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi unaotegemea maarifa, teknolojia, ubunifu na nguvu kazi yenye ujuzi wa hali ya juu.


Kasore alisema VETA inaendelea kupitia mitaala yake ili kuingiza zaidi matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Mnemba (AI), teknolojia za kidijitali na ujuzi unaohitajika katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, ili wahitimu waweze kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.


Alisema katika kufanikisha Dira ya 2050, mafunzo ya ufundi yanapaswa kuendelea kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kutatua changamoto za uzalishaji, kuongeza thamani ya bidhaa, kuanzisha biashara na kuajiri wengine, badala ya kutegemea ajira za ofisini pekee.


Aidha, alisema VETA itaendelea kuimarisha utambuzi wa ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu ili kuwapa nafasi watu wenye ujuzi wa vitendo kupata vyeti vinavyotambulika na kuongeza ushindani wao katika soko la ajira.


Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), Dkt. Andrew Boy, alisema chuo hicho kina jukumu la kimkakati la kuandaa wakufunzi wa elimu ya ufundi watakaofundisha katika vituo vya VET nchini.


Alisema wakati Serikali ikiendelea kupanua elimu ya amali katika shule na kuimarisha elimu ya ufundi, mahitaji ya wakufunzi yataendelea kuongezeka, hivyo chuo kinaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia, mitaala na mbinu za ufundishaji ili kuzalisha wakufunzi wenye umahiri unaokidhi mahitaji ya sasa.


"Ubora wa elimu ya ufundi unaanza na ubora wa mkufunzi. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika kuwaandaa wakufunzi watakaoweza kutumia teknolojia mpya na kufundisha kwa kuzingatia mahitaji halisi ya soko la ajira," alisema.


Kwa upande wake, Mwenyekiti aliyemaliza muda wa Baraza la Uongozi la MVTTC, Prof. Zakaria Mganilwa, alisema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake yametokana na ushirikiano kati ya Serikali, menejimenti ya chuo na wadau wa elimu ya ufundi.


Aliwataka wajumbe wa Baraza jipya kuendeleza juhudi za kuimarisha ubora wa mafunzo, kuongeza ushirikiano na sekta binafsi na kuhakikisha MVTTC inaendelea kuwa kitovu cha kuzalisha wakufunzi wenye uwezo wa kuandaa nguvu kazi itakayochangia maendeleo ya Taifa.


Alisema mabadiliko ya teknolojia yanahitaji taasisi za elimu kuendelea kufanya maboresho ya mara kwa mara ili wahitimu wanaozalishwa waendane na mahitaji halisi ya dunia ya kazi na kuchangia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.


Mwisho

No comments: