![]() |
![]() |
Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema uzembe wa dereva wa lori aina ya FAW ndio chanzo cha ajali ya kugongana uso kwa uso na lori la Scania katika eneo la Mafiga, iliyosababisha mtu mmoja kuteketea kwa moto na wengine wawili kujeruhiwa.
Ajali hiyo imetokea eneo la Mafiga, barabara kuu ya Morogoro–Iringa, Manispaa ya Morogoro na imehusisha lori lililokuwa limebeba mchanga aina ya FAW lililokuwa likitoka Lugono Morogoro kuelekea Chalinze na lori aina ya Scania lenye namba T 7328 DQD likikokota tela namba T 703 DVQ lililobeba kemikali aina ya sulphur kutoka Dar es Salaam kuelekea Congo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, lori hilo la FAW limegongana uso kwa uso na Scania hiyo baada ya dereva wake kuhama upande wake kabisa, kabla ya lori hilo kushika moto.
![]() |
Mtu mmoja aliyekuwa ndani ya lori la mchanga amefariki dunia baada ya kuteketea kwa moto, huku dereva wa Scania, Godfrey Samson Mushi, mwenye umri wa miaka 42, pamoja na utingo wake Meshack Mushi, miaka 24, wakijeruhiwa.
Abdul Kamga, mkazi wa eneo hilo, anasema ajali hiyo inapaswa kuwa fundisho kwa madereva wanaoendesha magari kwa safari ndefu, akisisitiza kuwa uchovu unaweza kupunguza umakini wa dereva.
"Madereva wanapohisi wamechoka au usingizi unawapata, wasilazimishe kuendelea na safari. Ni bora waegeshe magari sehemu salama na wapumzike mpaka watakapokuwa tayari kuendelea," anasema Kamga.
Amesema kuchukua mapumziko kwa wakati kunaweza kusaidia dereva kurejesha umakini na kupunguza uwezekano wa kusababisha ajali.
Kwa upande wake, Juma Msangi, shuhuda wa ajali hiyo, amesema wananchi wanashtushwa na kishindo kikubwa kabla ya kukimbilia eneo la tukio.
"Tuliposikia kishindo tulikimbilia eneo la tukio na kukuta malori yamegongana. Moja lilikuwa limeanza kuwaka moto na wananchi walikuwa wakijaribu kusaidia," anasema Msangi.
"Hali ilikuwa ya kutisha kwa sababu moto ulikuwa ukiwaka kwenye lori. Watu walikusanyika na kila mmoja alikuwa akijaribu kuona namna ya kusaidia," anasema Peter Emil, shuhuda mwingine
![]() |
| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo |
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa dereva wa lori aina ya FAW alisababisha ajali hiyo baada ya kujaribu kuhama upande wake bila kuchukua tahadhari.
Akawataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuepuka vitendo vya uzembe, ikiwemo kuendesha kwa mwendo usio salama na kufanya uendeshaji wa hatari wa kupita magari.
Kamanda Kantimbo pia amewataka madereva wanaosafiri umbali mrefu kuhakikisha wanapata muda wa kutosha wa kupumzika na kutokuendesha wanapokuwa wamechoka au kusinzia.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa 11 alfajiri na kusababisha taharuki kwa wananchi wa Mafiga, huku moja ya malori likiteketea kwa moto na kemikali aina ya sulphur iliyokuwa ikisafirishwa kumwagika katika eneo la tukio.
Tukio hilo linaendelea kufanyiwa uchunguzi na mamlaka husika ili kubaini kwa kina mazingira yote yaliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo.
Mwisho.





No comments:
Post a Comment