Mwandishi wetu, Maipac Ludewa
maipacarusha20@gmail.com
Wananchi wa Kijiji cha Mkongobaki, Kata ya Mkongobaki, wameiomba Serikali kuhakikisha eneo lililotengwa awali kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari katika kata hiyo linaendelea kuwa na matumizi ya kiserikali, baada ya shule kujengwa katika Kijiji cha Ugera.
Ombi hilo limetolewa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, wakati wa mkutano uliofanyika Kijiji cha Mkongobaki, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa kata hiyo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya alifanya mikutano ya hadhara katika vijiji vya Mkongobaki, Ugera na Lipangala kuzungumza na wananchi kupokea kero zao.
Wananchi hao wameeleza kuwa hawataki eneo walilolitoa kwa ajili ya ujenzi wa shule libaki bila matumizi ya umma, hivyo wakaiomba Serikali kulipatia matumizi mengine yatakayowanufaisha wakazi wa kata hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Olivanus Thomas amependekeza eneo hilo lijengwe Shule ya Sekondari ya kidato cha tano na Sita , huku akieleza kwamba wazo hilo alikuwa akilitafutia nafasi ya kulitekeleza kwa manufaa ya wananchi wa Kata ya Mkongobaki.
Amesema kuwa shule ya sekondari ya kata tayari imejengwa, nasasa ni wakati wa wananchi kushirikiana kuhakikisha eneo hilo linatumika kujenga shule ya sekondari kidato cha tano na cha sita ili kuongeza fursa za elimu kwa vijana wa eneo hilo.
"Hili ni pendekezo, tushirikiane kulijadili ili tupate uamuzi wa pamoja utakaowanufaisha wananchi wote wa kata ya Mkongobaki," amesema Thomas.
Ili kufikia maamuzi ya maridhiano, Thomas ameunda timu ya wajumbe 30, ikijumuisha wajumbe 10 kutoka kila kijiji cha Mkongobaki, Ugera na Lipangala, watakaokutana kujadili na kupendekeza matumizi sahihi ya eneo hilo.
Ameeleza kuwa lengo la timu hiyo ni kuhakikisha uamuzi unaofikiwa ukizingatia maslahi ya kata nzima na kumaliza tofauti za muda mrefu zilizotokana na ujenzi wa Shule ya Sekondari Ugera.
"Ifike mahali tulimalize kabisa suala hili la sekondari na tuendelee kujenga umoja pamoja na kuharakisha maendeleo ya wananchi wetu yanapatikana," amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Wananchi walioshiriki mkutano huo walilipokea pendekezo hilo, wakisema ujenzi wa shule ya kidato cha tano na cha sita katika eneo hilo utakuwa suluhisho la kudumu na utaleta manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Edison Luoga na Jackson Mhagama waliipongeza Serikali kwa hatua ya kutafuta suluhisho la kudumu, wakiahidi kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hatua hiyo inatarajiwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu uliokuwepo kati ya Kijiji cha Mkongobaki na vijiji vingine vya Kata ya Mkongobaki kuhusu eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari, huku matarajio yakielekezwa kwenye ujenzi wa Shule ya Kidato cha tano na Sita katika eneo hilo endapo wananchi wa kata hiyo watafikia maridhiano ya pamoja.


No comments:
Post a Comment