Mbunge Shayo akabidhi ambulance kutekeleza ahadi kwa wananchi wa Moshi Mjini - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 25 July 2026

Mbunge Shayo akabidhi ambulance kutekeleza ahadi kwa wananchi wa Moshi Mjini

 




Na Mwandishi Wetu


maipacarusha20@gmail.com 


Moshi. Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Ibrahim Shayo, ametekeleza moja ya ahadi zake za uchaguzi kwa kukabidhi rasmi gari la kubebea wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Manispaa ya Moshi.


Ambulance hiyo imezinduliwa leo Julai 25 na Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, aliyempongeza mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi zake kwa wakati na kusema hatua hiyo ni mfano wa uongozi unaowajibika kwa wananchi.


Uzinduzi huo umefanyika katika Uwanja wa Michezo wa Majengo, Manispaa ya Moshi, sambamba na hafla ya kukabidhi magari yatakayotumika katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi binafsi za mbunge huyo kwa wananchi wa jimbo lake.


"Nimpongeze Mbunge wa Moshi Mjini kwa kutekeleza ahadi zake kwa wakati. Hii ni ishara ya uongozi wa kuwajibika. Wabunge wengi hutoa ahadi nyingi wakati wa kampeni, lakini utekelezaji wake huwa wa kusuasua au hausikiki kabisa hadi uchaguzi unapokaribia tena," alisema Mchengerwa.


Alisema kutotekelezwa kwa ahadi kunachangia mabadiliko makubwa ya wabunge baada ya kila uchaguzi mkuu.


"Kila baada ya miaka mitano kati ya asilimia 65 hadi 75 ya wabunge wanaoingia Bungeni huwa ni wapya. Mwaka 2015 wabunge wapya walikuwa asilimia 87, mwaka 2020 walikuwa asilimia 70 na mwaka 2025 wamefikia asilimia 68. Hii inaonyesha wananchi wanawawajibisha viongozi wanaoshindwa kutimiza ahadi zao," alisema.


Akizungumza katika hafla hiyo, Shayo alisema aliahidi wakati wa kampeni kuwa, mbali na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, angekuwa na ahadi binafsi ambazo angezitekeleza kwa kutumia uwezo na rasilimali zake mwenyewe.


Alisema miongoni mwa ahadi hizo ni kutoa magari mawili aina ya Coaster yatakayosaidia shughuli za kijamii, pamoja na ambulance na gari la kubebea miili kwa ajili ya kuwahudumia wananchi katika nyakati mbalimbali za uhitaji.


"Moja ya ahadi nilizotoa ilikuwa kuwa karibu na wananchi wakati wote. Leo ninafurahi kuona ahadi hizi zimeanza kutekelezwa kwa vitendo kwa manufaa ya wananchi wa Moshi Mjini," alisema Shayo.


Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema utekelezaji wa ahadi hizo unaonyesha dhamira ya kweli ya mbunge huyo katika kuwahudumia wananchi.


"Ninatoa pongezi kwa Mbunge wetu kwa kutimiza alichowaahidi wananchi. Hii ni hatua inayostahili kuigwa na viongozi wengine kwa sababu wananchi wanathamini matendo kuliko maneno," alisema.


Naye Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, alisema magari hayo ni sehemu ya ahadi binafsi za mbunge huyo ambazo hazikuwa sehemu ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM.


"Haya ni mambo ambayo Mbunge wetu aliamua kuyafanya kwa hiari yake ili kuongeza huduma kwa wananchi. Leo tunashuhudia utekelezaji wake kwa vitendo, jambo linaloonyesha uadilifu na uwajibikaji kwa wananchi waliomchagua," alisema.

No comments: