Burhani Yakub,Tanga.
maipacarusha20@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Dkt Balozi Batilda Burian ameipa wiki mbili timu aliyounda wakati wa kikao cha kujadili namna bora ya kukitumia kituo kikuu cha mabasi cha Kange Jijini Tanga.
Timu hiyo ya wataalamu kutoka ofisi yake na Halmashauri ya Jiji la Tanga ilikusanya maoni yaliyotolewa na wadau wa usafirishaji, wananchi ,mbunge wa Jimbo la Tanga na viongozi mbalimbali katika kikao kilichofanyika leo Julai 25 .
Kikao hicho amekiitisha kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa mgogoro uliobuka huvi karibuni baada ya zoezi lililopangwa Julai 15 mwaka huu na Halmashauri ya Jiji la Tanga la kuhakikisha mabasi yote yanayofanya safari kwenda mikoani yaanzie kituo kikuu cha mabasi cha Kange kukwama.
Baada ya kukwama kwa zoezi hilo Meya wa Jiji la Tanga, Mustapher Mhina (Selebosi) alisema haoni busara kuacha fedha za Serikali zilizotumika kujenga kituo kikuu cha mabasi cha Kange pamoja na jengo la kitega uchmi zikipotea bila kutumika.
Alisema kutokana na kukwama kwa kutumika kituo hicho kamati ya fedha ya Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Jiji walipendekeza kibadilishwe matumizi badala yake kitumike kuegesha maroli.
Juzi viongozi wa chama cha wamiliki wa mabasi (Taboa),Chemba ya wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo ( TNCC) na Jumuiya ya wafanyabiashara wadogo (JWT) wakizungumza na waandishi wa habari kuhhusiana na sakata hilo na kueleza kuwa wenye mabasi hawajakataa kutumia kituo cha Kikuu cha mabasi cha Kange bali maboresho waliyopendekeza hayakufanyika.
Katika kikao hicho na waandishi wa habari wamiliki wa mabasi waliomba kupewa miezi sita ya kufanyika kwa maboresho mapungufu yaliyopo katika kituo kikuu cha mabasi cha Kange huku nao wakijenga terminal katikati ya mji ili kuondoa msongamano uliopo katika barabara ya 12 ,13 na 14 Jijini Tanga.
Katikati kikao kilichofanyika leo wadau wa usafirishaji wametoa mapendekezo ya namna bora ya kukitumia kituo kikuu cha mabasi cha Kange huku wakisistiza kwamba hawako tayari kushuhudia kikibadilishiwa matumizi.
Mbunge wa Jimbo la Tanga,Kassim Mbarouk(Makubel) amesema kituo cha Kange kimewekwa eneo sahihi hasa ikizingatiwa kuwa mji unapanuka kwa kasi na kwamba baadaye kitakuwa ni katikati kutokana na barabara ziatazojengwa.
Amewataka wadau wa usafirishaji kuondoa hofu kuhusu kituo kikuu cha mabasi cha Kange badala yake watoe ushirikiano ili kuiwezesha Halmashauri kukusanya mapato makubwa.
Mmilki wa kampuni ya mabasi ya Ratco, Mohamed Salim ameitaka Halmashauri ya Jiji la Tanga kuacha kuwakwamisha wenye mabasi kwa kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi.
Akizungumza wakati akifunga kikao hicho,Mkuu wa mkoa wa Tanga,Dkt Burian amesema kazi itakayofanywa na timu ya wataalamu ni kuyachakata maoni yote yaliyotolewa ambapo baada ya wiki mbili atakutana na wadau hao ili kujadili njia ya kutumika .
"Timu ya wataalamu iliyokuwa ikiandika maoni haya tunaipa muda wa kuyachakata na kisha tutaitana kama hivi ili tuangalie ni njia ipi sasa twende nayo kuhakikisha kituo hicho Kikuu cha mabasi cha Kange kinatoa huduma bora kwa wananchi.
Kituo kikuu cha mabasi cha Kange kilianza kujengwa mwaka 2012 na kukamillika mwaka 2014 kwa fedha kutoka Serikali Kuu kupitia mradi wa uboreshaji wa miji (TSCP) kiasi cha takribani.Sh 6.8bilioni wakati jengo la kitega uchumi ujenzi wake ulianza mwaka 2019 na kukamilika mwaka 2023 kwa fedha kutoka serikali kuu likigharimu 8.76bilion.
MWISHO

No comments:
Post a Comment