Na Mwandishi wetu, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema Wilaya ya Arusha imekamilisha maandalizi yote ya kuupokea Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2026 utakaowasili kesho Julai 9, 2026 saa 1:30 asubuhi katika Viwanja vya Magereza Kisongo, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi hayo na shughuli zote zitakazoambatana na mbio za Mwenge.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Mkude alisema Mwenge wa Uhuru utaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji na mshikamano wa wananchi kupitia ukaguzi, uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi.
Alisema katika safari yake ndani ya Wilaya ya Arusha, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Tarafa za Themi, Suye na Elerai, ukipitia kata saba kati ya kata 25 za wilaya hiyo kwa umbali wa kilometa 89.2.
Mkude alisema Mwenge huo utazindua miradi miwili, utaweka mawe ya msingi katika miradi mitatu na kutembelea miradi miwili, yote ikiwa na thamani ya Shilingi 3,906,458,896.79. Kati ya fedha hizo, Shilingi 677,597,123.30 zimetolewa na Serikali Kuu, Shilingi 2,979,611,773.49 na Halmashauri, huku wananchi wakichangia Shilingi 249,250,000.
Alisema miradi hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia uwekezaji katika sekta muhimu za maendeleo.
Alitaja miradi itakayopitiwa na Mwenge kuwa ni ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 katika eneo la Kimandorosi, ujenzi wa Shule ya Msingi Murieti iliyojengwa kwa mfumo wa ghorofa, jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Moivaro, mradi wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Arusha, mradi wa ufugaji wa kuku wa mayai unaoendeshwa na sekta binafsi pamoja na ujenzi wa barabara ya Giliki katika Kata ya Sakina.
Akizungumzia mradi wa barabara ya Giliki, Mkude alisema awali fedha zilizotengwa zilitosha kujenga kilomita 1.1 pekee kati ya kilomita 1.7 zilizohitajika, lakini Halmashauri ya Jiji la Arusha ilitoa fedha za ziada kukamilisha sehemu iliyobaki kwa kushirikiana na wananchi. Alisema hatua hiyo imeonesha namna ushiriki wa wananchi unavyochangia mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kuhusu Shule ya Msingi Murieti, alisema imejengwa kwa mfumo wa ghorofa ili kutumia vizuri eneo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa ardhi katika maeneo ya mjini, huku akibainisha kuwa ubunifu huo utasaidia kuongeza nafasi za kujifunzia bila kuhitaji eneo kubwa.
Mkude alisema pamoja na kukagua miradi ya maendeleo, Mwenge wa Uhuru utaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya UKIMWI, malaria, rushwa, matumizi ya dawa za kulevya na utunzaji wa mazingira, sambamba na kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo."
Aidha, alisema baada ya shughuli za mchana kukamilika, kutafanyika mkesha wa Mwenge wa Uhuru katika Viwanja vya FFU Mworombo, utakaoambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Ali Kiba na Juma Nature, huku akiwakaribisha wananchi kujitokeza kushiriki.
Akihitimisha, Mkude alisema Wilaya ya Arusha ipo tayari kwa asilimia 100 kuupokea Mwenge wa Uhuru na kwamba matarajio ni kuona wananchi wakijitokeza kwa wingi kuushuhudia, kutembelea miradi ya maendeleo na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.

No comments:
Post a Comment