POLISI MOROGORO WAONYESHA UZALENDO KWA KUCHANGIA DAMU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 24 July 2026

POLISI MOROGORO WAONYESHA UZALENDO KWA KUCHANGIA DAMU

 




 


Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com 


Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kupitia Kitengo cha Polisi Jamii limeendelea kuonesha dhamira yake ya kuhudumia jamii kwa kushiriki zoezi la uchangiaji damu, likilenga kuongeza akiba ya Benki ya Damu na kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo. 


Zoezi hilo lilifanyika katika eneo la Stendi ya Zamani ya daladala Manispaa ya Morogoro.


Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro, SSP Osca Ngumbulu, aliwapongeza askari wote waliojitokeza kuchangia damu kwa kujitolea kuokoa maisha ya wengine. 


Pia aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo ili kuongeza akiba ya damu katika Benki ya Damu na kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa wagonjwa wenye uhitaji.


Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Morogoro, SP Richard Mkesi, ambaye alikuwa mratibu wa zoezi hilo, alisema ushiriki wa Kitengo cha Polisi Jamii ni sehemu ya shughuli za kijamii kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Polisi Jamii. 


Alieleza kuwa hatua hiyo inaakisi dhamira ya Jeshi la Polisi ya kuendelea kuhudumia na kushirikiana na jamii. 


Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuimarisha usalama katika maeneo yao.


Naye Mtaalamu wa Maabara, Bensonatus Henerco, alilipongeza Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Polisi Jamii Wilaya ya Morogoro kwa kujitolea kushiriki zoezi hilo. 


Alisema damu inayochangwa ni msaada muhimu kwa wagonjwa mbalimbali, wakiwemo waathirika wa ajali, wajawazito na wagonjwa wenye magonjwa yanayohitaji kuongezewa damu. Pia alivitaka vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi mbalimbali kuiga mfano huo kwa kushiriki shughuli zinazolenga kuokoa maisha ya wananchi.


Kwa upande wao, maafisa usafirishaji pamoja na wananchi Denis Harun, Nassoro Ndege na Khamis Mkumbi waliwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika zoezi la uchangiaji damu kila linapoandaliwa. Walisema mbali na kuokoa maisha ya wengine, uchangiaji damu huwapa washiriki fursa ya kufahamu hali zao za afya kupitia vipimo vinavyofanyika kabla ya kuchangia damu.


Mwisho..

No comments: