SAKATA LA STENDI YA KANGE TANGA LACHUKUA SURA MPYA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 24 July 2026

SAKATA LA STENDI YA KANGE TANGA LACHUKUA SURA MPYA

 



Burhani Yakub,  Tanga 


maipacarusha20@gmail.com 


Sakata la kutumia kituo kikuu cha mabasi cha mkoa wa Tanga cha Kange limeingia sura mpya baada ya chama cha  wamiliki Taboa, jumuiya ya wafanyabiashara ndogo (JWT) pamoja na chemba ya wafanyabiashara,wenye viwanda na kudai hawajakataa kupakia abiria.


Badala yake wametaka utaratibu wa awali uendelee kutumika huku wakiomba  kupewa miezi sita ya kujenga terminal zao katikati ya mji na  Halmashauri ya Jiji la Tanga ifanyie maboresho kituo kikuu cha mabasi cha Kange ili kiwe na huduma rafiki kwa abiria.


Wametoa msimamo huo leo wakati wakizungumza na waandishi wa habari baada ya Meya wa Jiji la Tanga, Mohamed Mustapher (Selebosi) kukaririwa akielezea maamuzi ya kikao cha kamati ya fedha ya Baraza la madiwani kutishia kugeuza matumizi ya kituo hicho kuwa cha kuegesha maroli.


Wamesema wamiliki wa mabasi hawajakataa kukitumia kituo kikuu cha mabasi cha Kange na ndiyo maana mabasi yao yamekuwa yakipitishwa hapo kabla ya kuanza safari ya kuelekea na kurejea kutoka mikoani.



Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) mkoa wa Tanga, Albert Peter amesema wao pamoja na wananchi wamepatwa na taharuki baada ya kusikia kuwa kituo kikuu cha mabasi cha Kange kinabadilishwa matumizi kwa kuwa hawajawahi kukataa kukitumia.


"Tulikaa na uongozi wa Halmashauri tukaomba kifanyiwe maboresho ikiwamo kuwekwa vikalio vya abiria wakati wakisubiri kupanda mabasi,kuwekwa japo kituo cha kutolea huduma ya kwanza,kituo cha polisi na kuboresha kituo cha daladala lakini hadi sasa halijafanyika"amesema Albert.


Meneja wa Chemba ya wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo (TNCC) mkoa wa Tanga,Charles Hoza amesema wameamua kuingilia kati sakata hilo baada ya viongozi wa Taboa na JWT kuomba yafanyike mzungumzo ili upatikane ufumbuzi.


Naibu katibu wa Taboa mkoa wa Tanga, Hassan Hashim amesema chanzo cha sakata hilo ni Halmashauri kupiga marufuku mabasi kupakiza abiria kwenye terminal zake zilizopo katikati ya mji na kuamrisha safari ianzie kituo kikuu cha Kange.


"Sisi hatujakataa kwani baada ya kutoka kwenye terminal zetu ambazo zina huduma zote muhimu na za kisasa za abiria mabasi yetu lazima yapitie kituo kikuu cha Kange na kulipa tozo zote ikiwamo kukaguliwa na Trafiki na Latra...tumeshangazwa kusikia kusikia tumegoma   hii si kweli"amesema Hashim.


Katibu wa Jumuiya ya wafanyabiashara wadogo JWT mkoa wa Tanga, Ismail Masoud amesema katika kikao chao na wamiliki wa mabasi ili kuondoa msongamano wa mabasi katikati ya mji,wamekubaliana kuomba wapewe miezi sita wasio  na terminal wajenge huku Halmashauri nayo ikifanyia maboresho mapungufu yaliyopo kituo kikuu cha mabasi cha Kange.


"Katika kipindi hiki cha miezi sita utaratibu uliopo sasa uendelee kutumika lakini kitakapomalizika tusione basi lolote likitumia barabara za namba kupakia au kushusha abiria na kila mmiliki awe na terminal yake aisyekuwa nayo aanzie safari kituo kikuu cha Kange na hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaokiuka"amesema Masoud.


Hatua hiyo imefikiwa baada ya Selebosi na baadhi ya madiwani kunukuliwa na vyombo vya habari wakielezea maamuzi ya kikao cha kamati ya fedha ya Halmashauri ya Jiji la Tanga ya kugeuza matumizi ya kituo kikuu cha mabasi cha Kange na kuwa maegesho ya maroli.


"Licha ya kukaa na wamiliki wa mabasi,Latra na jeshi la polisi kukubaliana na baadaye kutumia fedha za Halmashauri kupita na gari la matangazo mji wote kutangaza kwamba ifikapo Julai 15 mabasi yote yaendayo mikoani yaanzie safari kituo cha Kange... wakati tunaanza kutekeleza siku hiyo hiyo ghafla unasitishwa bila kushirikishwa"amesema Selebosi.


Meya huyo amesema haoni busara  Serikali imetumia fedha nyingi kujenga kituo kikuu cha mabasi cha Kange na jengo la kitega uchumi lenye huduma zote kwa lengo la kutumika ili wananchi wanaufaike halafu lisitumike kama lilivyokusudiwa 


       MWISHO

No comments: