Na Julieth Mkireri, Maipac Mafia
maipacarusha20@gmail.com
Timu ya Maafa ya Wilaya ya Mafia imewaokoa abiria 22 ambao ni raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na visiwa vya Comoro walionusurika kifo baada ya boti waliyokuwa wamepanda kutokea Comoro kwenda kisiwa cha Mayotte kupata hitilafu na kushindwa kufika kisiwa hicho.
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Mafia Aziza Mangosongo amesema raia hao waliokolewa Julai 22, 2026 katika fukwe za kijiji cha Kungwi kilichopo kata ya Baleni baada ya boti waliyokuwa wamepanda yenye ukubwa wa H40 yenye mashine aina ya "YAMAHA" isiyokuwa na usajili kushindwa kufika kisiwa cha Mayotte kutokana na hitilafu waliyopata.
Boti hiyo ilitoka Comoro ikiwa na abiria 36 ambao abiria 14 kati ya hao walifariki njiani mara baada ya boti kupata hitilafu.
Mangosongo ameeleza kuwa raia hao walikuwa na lengo la kufika nchi ya Ufaransa kwa urahisi kutokea kisiwa hicho cha Mayotte kwa lengo la kuepuka vurugu kutoka katika nchi zao pamoja na kutafuta maisha mazuri barani Ulaya.
Uongozi wa Wilaya ya Mafia kwa kushirikiana na timu ya maafa ya Wilaya na wadau mbalimbali umewapatia msaada wa nguo na chakula manusura hao ambao tisa kati yao ni wanaume, nane ni wanawake na watoto watano ( watatu ni wavulana na wawili ni watoto wa kike) ambapo hivi sasa wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya, Kilindoni.
Mangosongo ameishukuru Serikali ya kijiji cha Kungwi kwa kutoa taarifa kwa haraka, timu ya wataalam wa afya, timu ya maafa na wananchi wote kuhakikisha manusura hao wanapatiwa matibabu kwa wakati pamoja na huduma nyingine muhimu.
Aidha, amewataka wananchi kufanya kazi za halali na kufuata taratibu pale wanapotaka kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.


No comments:
Post a Comment