TARI Selian yawaalika wakulima kwenye maonesho ya kilimo-biashara, yahimiza matumizi ya mbegu na mazao bora ya lishe - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 10 July 2026

TARI Selian yawaalika wakulima kwenye maonesho ya kilimo-biashara, yahimiza matumizi ya mbegu na mazao bora ya lishe

 



Na Mwandishi wetu,Arusha


maipacarusha20@gmail.com 


Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Selian kimewataka Wakulima kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho ya kilimo-biashara yaliyoanza leo na kuendelea kwa siku mbili katika kituo hicho kilichopo Selian, Arusha.



Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa TARI Selian, Dkt. Caresma Chuwa, alisema mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla.


Dkt. Chuwa alisema maonesho hayo yatawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wasindikaji wa mazao, wajasiriamali pamoja na wadau wa mnyororo mzima wa thamani wa kilimo kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza teknolojia mpya za kilimo.


Alisema maonesho hayo pia yatatoa fursa kwa wakulima kujifunza mbinu bora za uzalishaji, usindikaji na masoko ili kuongeza tija na kipato kupitia sekta ya kilimo.



Dkt. Chuwa alisema lengo la maonesho hayo ni kuhakikisha mkulima anapata uelewa wa teknolojia mbalimbali za kisasa zitakazomwezesha kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya kilimo.

Alisema kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu ni, "Kabiliana na mabadiliko ya tabianchi, tumia teknolojia bunifu za kilimo kwa uhakika wa chakula na kipato."


Aidha, aliwahimiza Watanzania kutumia maharage ya lishe pamoja na mbegu bora za mahindi zilizofanyiwa utafiti na TARI Selian, ambazo tayari zinapatikana sokoni kwa matumizi ya wakulima.


Alieleza kuwa maharage na mahindi hayo yana virutubisho muhimu vinavyoweza kusaidia jamii kupata lishe bora na kuchangia kupunguza tatizo la utapiamlo nchini.


Kwa upande wake, Mratibu wa Maonesho ambaye pia ni Mratibu wa Teknolojia na Mashirikiano wa TARI Selian, Bi. Edith Kadege, alisema maandalizi ya maonesho hayo yamekamilika kwa asilimia 100.


Bi. Kadege aliwataka wakulima kutoka maeneo mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo ili kujifunza teknolojia mpya zinazoweza kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo.


Alisema matumizi ya teknolojia sahihi yanamwezesha mkulima kufanya kilimo kwa ufanisi mkubwa na kuachana na mbinu zisizo na tija ambazo zimekuwa zikikwamisha ongezeko la uzalishaji.


Aliongeza kuwa maonesho ya mwaka huu yana utofauti mkubwa na yale ya miaka iliyopita kutokana na uwepo wa teknolojia mpya pamoja na ubunifu mbalimbali utakaowasilishwa na waoneshaji, wakiwemo watafiti wa TARI Selian.


Bi. Kadege alisema waoneshaji hao watatoa elimu na kuonesha mbegu pamoja na teknolojia mpya zinazolenga kuongeza uzalishaji wa mazao, hivyo kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wakulima nchini.


Mwisho

No comments: