WALIMU WATAKIWA KUANDAA WAHITIMU WANAOJIAJIRI NA KUUNDA FURSA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 27 July 2026

WALIMU WATAKIWA KUANDAA WAHITIMU WANAOJIAJIRI NA KUUNDA FURSA

 

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo




Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo, amewataka walimu kutumia nafasi yao kuwajengea wanafunzi maarifa na ujuzi wa kujiajiri, kuajiri wengine na kutatua changamoto za maisha badala ya kuwaandaa kwa ajili ya kufaulu mitihani pekee.


Prof. Nombo alisema hayo mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa walimu wapya wa somo la Biashara watakaofundisha katika shule za sekondari za serikali nchini.


Alisema maboresho ya sera ya elimu na mitaala yaliyokamilika mwaka 2023 yanalenga kuzalisha wahitimu wenye ujuzi wa kujitegemea kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.


*"Jukumu la mwalimu si kumfundisha mwanafunzi kufaulu mtihani pekee, bali kumwezesha kutatua changamoto zinazomzunguka kwa kutumia mazingira yake na kubadili elimu yake kuwa chanzo cha kipato. Awe amesoma Chemistry, Biology au somo lolote, elimu yake lazima imsaidie kuboresha maisha yake," *alisema Prof. Nombo.*


Alieleza kuwa kupitia maboresho hayo, serikali imeanzisha mikondo miwili ya elimu ambayo ni elimu ya jumla na elimu ya amali, huku somo la Biashara likiwa la lazima katika mikondo yote kutokana na nafasi yake katika kukuza ujasiriamali na stadi za maisha.


Alisema mafunzo hayo yanakusudia kuwajengea walimu uwezo wa kutekeleza mitaala mipya kwa ufanisi ili kuwawezesha wanafunzi kutumia elimu yao kujenga uchumi binafsi na wa taifa.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Aneth Komba, alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na shirika la Educate inaendelea kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha somo la Biashara kwa kuzingatia mahitaji ya mitaala mipya.


Alisema katika awamu hiyo walimu wapya 702 wanapatiwa mafunzo ya siku tatu yatakayowawezesha kufundisha somo la Biashara kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule za sekondari za serikali.


*"Mafunzo haya yanawajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji, kuandaa maandalizi ya kazi na kutekeleza mitaala mipya kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyowekwa,"* alisema Dk. Komba.


Aliongeza kuwa lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanahitimu wakiwa na maarifa na ujuzi wa kujiajiri au kuanzisha ajira kwa wengine.


Dk. Komba alisema TET tayari imeshawafikia walimu zaidi ya 1,500 kupitia mafunzo hayo, huku awamu nyingine ikitarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti kwa walimu wa kujitolea watakaofundisha somo la Biashara katika shule mbalimbali za serikali.


Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri pamoja na viongozi wa shule kuwapa ushirikiano na usimamizi wa karibu walimu hao ili kuhakikisha ufundishaji wa somo la Biashara unaleta matokeo yaliyokusudiwa.


Naye Prof. Nombo alisisitiza kuwa mafanikio ya mageuzi ya elimu yatategemea weledi wa walimu katika kutekeleza mitaala mipya na kuhakikisha kila mwanafunzi anahitimu akiwa na maarifa, stadi na uwezo wa kutumia elimu yake kujiletea maendeleo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.


Mwisho.

No comments: