Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi limeanza maandalizi ya mkakati wa kukusanya na kuhifadhi mbegu za asili zinazokaribia kutoweka, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa chakula nchini na kuhifadhi urithi wa kilimo kwa vizazi vijavyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa **M&I Nane Nane JKT Club** katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Morogoro, Mkuu wa Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Rashid Mabena alisema mbegu hizo zitafanyiwa tafiti na kuboreshwa ili zitumike na wakulima wadogo, wa kati na wakubwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuwa na mbegu bora za Kitanzania.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na usalama wa chakula, hasa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
*"Kwa kufanya hivyo tutakuwa na uhakika wa chakula kwa ajili ya kulisha kizazi kijacho, huku tukihakikisha Watanzania wanapata chakula salama,"* alisema.
Brigedia Jenerali Mabena alisema pamoja na jukumu la ulinzi, JKT linaendelea kuwekeza katika shughuli za uzalishaji mali ili kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Alisema kuanzishwa kwa **M&I Nane Nane JKT Club** kutatoa huduma za vyakula na vinywaji kwa wananchi watakaotembelea maonyesho ya Nane Nane.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha JKT 832, Kanali George Barongo, alisema katika Maonyesho ya Nane Nane mwaka huu, JKT itaonesha na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo vyakula vya asili vya Kitanzania na vya mataifa mengine.
Aidha alisema banda la JKT litatoa elimu kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwawezesha wananchi kupata maarifa yatakayowaongezea tija katika shughuli zao.
Naye Meja Emmanuel Musa Shing'oma alisema maandalizi ya ushiriki wa JKT katika Maonyesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yamefikia hatua za mwisho, huku vifaa na bidhaa mbalimbali zikiendelea kuwasili.
Aliwahimiza wananchi kutembelea banda la JKT ili kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na jeshi hilo pamoja na kunufaika na huduma zitakazotolewa.
Mwisho..


No comments:
Post a Comment