Na Mwandishi wetu, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Fakii Lulandala amewasihi wakulima, wafugaji na wavuvi kushiriki maonyesho ya kilimo nane nane ili kuongeza ujuzi na kufanya shughuli zao kwa tija.
DC Lulandala akizungumza leo Ijumaa Agosti 7, 2026 baada ya kukagua baadhi ya mabanda ya maonyesho hayo ya kanda ya kaskazini yanayoendelea katika eneo la Themi jijini Arusha.
Amesema wakulima, wafugaji na wavuvi wakishiriki kwenye maonyesho hayo watapata fursa ya kukutana na wataalamu na kuweza kuongeza ujuzi katika shughuli zao.
"Nawapongeza sekretarieti ya maonyesho haya kwa kuandaa vyema kwani wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wengine wameshiriki na kupata ujuzi, ubunifu na kujifunza upya kufanya shughuli zao za uzalishaji kiuchumi kwa tija," amesema DC Lulandala.
Amesema kilimo, ufugaji na uvuvi ukifanyika kwa kufuata maelekezo ya wataalamu, utafanyika kwa tija na jamii kunufaika zaidi kiuchumi kuliko kufanya kazi kwa mazoea.
"Japokuwa tupo mwishoni mwa maonyesho hayo ya nane nane nawasihi wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi kushiriki ili kupata elimu kwa wataalamu juu ya namna ya kuboresha shughuli zao," amesema DC Lulandala.
Mmoja kati ya wajumbe wa sekretarieti wa maonyesho hayo, Samwel Dahaye amemweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa watu wengi wamehamasika kushiriki nane nane.
"Maonyesho haya ni ya kanda ya kaskazini kuna wakulima, wafugaji na wavuvi wametoka maeneno mbalimbali ikiwemo Babati na Hanang', Arumeru na Same," amesema Dahaye.
Mwenyekiti wa chama cha walimu nchini (CWT) wilaya ya Simanjiro, Mwalimu Abraham Kisimbi amesema maonyesho hayo ni mazuri kwani hata wanafunzi wanatembelea kupata elimu mbalimbali.
"Tumeona wanafunzi wa shule tofauti za mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, wakishiriki maonyesho hayo ya kilimo, mifugo na uvuvi, wakiuliza maswali na kupatiwa majawabu," amesema mwalimu Kisimbi.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya maonyesho hayo ya kilimo nane nane ni 'Tambua soko, ongeza tija kutekeleza Dira 2050.
MWISHO

No comments:
Post a Comment