![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Manyara Quine Sendiga akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya mazingira mabadiliko ya tabianchi na watetezi wa haki za binaadamu Manyara |
Mussa Juma, Babati
maipacarusha20@gmail.com
Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) kwa kushirikiana na wadau wake, kimezindua ripoti ya mazingira, mabadiliko ya tabia nchi na watetezi wa haki za mazingira kwa mkoa wa Manyara, ambayo imebaini mambo kadhaa, ikiwepo uwepo wa hatari za kimazingira kwa Jamii hasa za asili na Mazingira magumu kwa Watetezi wa haki za Mazingira.
Ripoti hiyo ni sehemu ya Mradi wa Kikanda uliolenga kuimarisha ushiriki wa Jamii za Asili, Asasi za Kiraia, Mitandao, Watetezi wa Haki za Mazingira katika shughuli za uhifadhi na hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaotekelezwa katika Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda kuanzia mwaka 2024-2027 ukifadhiliwa na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Maendeleo (International Development Research Center (IDRC).
![]() |
Miongoni mwa yaliyobainika katika ripoti hiyo iliyowashirikisha watu 504, uwepo wa Athari kubwa za kimazingira ambazo zimetokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwepo Ukame, mafuriko, Maporomoko ya ardhi, kuanguka kwa miamba na tope na ukataji miti.
Ripoti hiyo pia imebaini upungufu wa Maji, Chakula na Malisho kwa maeneo ya jamii za asili, ushindani wa matumizi ya ardhi na rasilimali maji kuongezeka, na uwepo wa migogoro baina ya wakulima, wafugaji na jamii nyingine za asili.
LHRC katika ripoti hiyo, wamebainisha kuwa imebainika kuongezeka mazingira ya hatari kwa jamii za asili, vikwazo katika ushiriki wa kiraia inavyoathiri kwa kiwango kikubwa zaidi kwa jamii za wachache na jamii za asili.
Ripoti hiyo, ambayo tayari imekabidhiwa serikali na kwa wadau wa mazingira pia imebainisha watetezi wa haki za mazingira wanaendelea kukabiliwa na hatari au changamoto mbali mbali wanapotimiza majukumu yao, ikiwepo vitisho, kunyanyaswa, kubughudhiwa kisheria na vitisho dhidi yao na wanafamilia.
![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Manyara Quine Sendiga akizindua ripoti ya mazingira, mabadiliko ya tabia nchi na watetezi wa haki za mazingira kwa mkoa wa Manyara |
Ripoti hiyo, Imezinduliwa na Julai 29, mwaka 2026, wilayani Babati na Mkuu wa mkoa wa Manyara, Qeen Sendiga na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vijiji kutoka katika wilaya za Kiteto na Hanang ulipofanyika utafiti huo, pia na viongozi wa serikali, Asasi za Kiraia na Watetezi wa Haki za Mazingira.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu huyo wa mkoa, alipongeza jitihada za LHRC katika masuala ya utetezi wa haki za binaadamu ikiwepo haki za mazingira zikiwepo jamii za pembezoni ambazo zipo hatarini zaidi.
![]() |
Sendiga amesema anakubaliana na taarifa za ripoti hiyo za uwepo wa changamoto za kimazingira kutokana na mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo imeanza kuathiri maisha ya wananchi wengi.
Amesema kwa jamii za asili kama Wahadzabe zinapitia kipindi kigumu, kwani ardhi yao inavamiwa na wakulima na wafugaji, hivyo kuanza kukosa matunda, mizizi na miti ambayo wanaweza kuweka mizinga nili kuvuna asali.
“Mara kadhaa nimetembelea jamii ya Wahadzabe wanalalamikia changamoto za mabadiliko haya ya tabia nchi, lakini sio jamii hiyo tu, Athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kubwa kwani hali ya hew ahata hapa Babati mjini imebadilika sana baridi imeongezeka “amesema
Akielezea ripoti hiyo,Afisa Utafiti, wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu(LHRC), Fundikila Wazambi anasema utafiti huo, umebaini uelewa wa haki za kiraia na haki za mazingira bado ni mdogo katika jamii.
“Ni asilimia 46 pekee ya washiriki walioelekeza kwamba wana uelewa wa kiwango Fulani kuhusu haki zao za kiraia huku asilimia 38 tu wakitambua nafasi na mchango wa watetezi wa mazingira”’ anasema
Amesema utafiti umebaini pia uelewa mdogo kuhusu haki za watetezi wa mazingira umeanza kutafsiriwa ni wapinga maendeleo jambo ambalo linachangia hofu na ukimya unaozuia wananchi kushiriki katika utetezi wa mazingira.
Wazambi anasema ripoti imebaini pia mifumo ya maarifa ya jadi una mchango mkubwa kayika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi kupitia usimamizi endelevu wa maeneo ya malisho, uhifadhi wa vyanzo vya maji,matumizi endelevu ya ardhi, na mbinu za kukabiliana na ukame.
“Ripoti imebainisha umuhimu wa kutambua, kuhifadhi na kuingiza maarifa ya jadi katika setra na program za kitaifa za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi”amesema
Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binaadamu(LHRC), Wakili Dk Anna Henga amesema ripoti imebaini watetezi wa haki za mazingira wana mchango mkubwa kayika kulinda rasilimali ,kuhimiza uwajibikaji na kuhakikisha mazingira yanalindwa na kutunzwa.
Wakili Dk Henga anasema anatoa wito kwa Serikali ya Tanzania na wadau kuimarisha mfumo wa kisheria na taasisi za ulinzi na utetezi wa mazingira,kukuza ushiriki jumuishi katika maamuzi yanayohusu mabadiliko ya tabia nchi,kuimarisha elimu ya haki za kiraia na iwepo wa mfumo Madhubuti wa msaada wa haraka kwa wanaokabiliwa na hatari.
“Wakati Tanzania ikiendelea kukabiliana na Athari za mabadiliko ya tabia nchi LHRC inasisitiza kwamba ulinzi endelevu wa mazingira hauwezi kufanikiwa bila kuwalinda wale wanaotetea mazingira,uwepo usalama wa ushiriki na utambuzi wa wadau wa mazingira”amesema
Meneja mwandamizi wa Ubora wa Programu(LHRC), Neema Sembeo anasema ripoti hiyo ni muhimu sana kwa Taifa kwani imebainisha changamoto za kimazingira na imekwenda mbali zaidi na kushauri utatuzi.
"Matokeo ya utafiti yameonesha jamii kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na kwa watetezi wa haki za mazingira hivyo ni muhimu kuwepo mikakati ya pamoja kukabiliana na changamoto hizi"anasema
Baadhi ya watetezi wa mazingira walioshiriki utafiti huo, Paulina Lenea na Maingapa Payai wakazi wa Partimbo wilaya ya Kiteto ,walisema bila hatua za dharura kuchukuliwa kulinda mazingira na kuwathamini watetezi wamazingira kutakuwa na Athari kubwa.
“Tunapeleka malalamiko kuhusu watu kukata miti na kuharibumazingira lakini hatua stahiki hazichukuliwi na sisi tunaonekana ni maadui”anasema Paulina.
Payai anasema kwa sasa jamii za asili ni waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi kwani ardhi yao inaendelea kuvamiwa na wakulima na watu wanaokata miti na kuchoma mikaa hivyo muhimu hatua kuchukuliwa.
Mkurugenzi wa shirika la Hanang Community Liberty Supporters Organisation (HALISO) lililopo wilaya ya Hanang, ambalo linajihusisha na utetezi wa mazingira ,Dominick Dancon anasema kuna umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano baina ya watetezi wa mazingira, serikali na wadau wengine kwani lengo lao ni moja kubwa ni kuhakikisha maziungira yanatunzwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Afisa Miradi wa shirika la Wanahabari la usaidizi wa jamii za Asili(MAIPAC), Andrea Ngobole anasema ili kuzilinda jamii za asili ni muhimu sasa serikali na wadau wa mazingira kuhakikisha ardhi ndogo iliyobaki ya jamii hizi kulindwa kisheria na kutolewa hati miliki lakini pia kuhakikisha uwepo wa mpango wa matumizi bora ya ardhi vijijini.
MWISH0









No comments:
Post a Comment