ELIMU YA MLIPAKODI YACHANGIA ONGEZEKO LA MAPATO YA TRA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 13 August 2026

ELIMU YA MLIPAKODI YACHANGIA ONGEZEKO LA MAPATO YA TRA

 





Burhani Yakub,Tanga.


maipacarusha20@gmail.com 


Elimu ya mlipakodi ambayo imekuwa ikitolewa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kupitia idara yake ya elimu kwa mlipakodi na mawasiliano imechangia ongezeko la ukusanyaji wa mapato.


Afisa Mkuu Msimamizi kodi wa idara ya elimu kwa mlipakodi na mawasiliano wa TRA,Salim Bakar ametoa taarifa hiyo leo wakati wa mafunzo ya mabadiliko ya sheria ya kodi ya mwaka 2026/27 yaliyotolewa kwa wafanyabiashara wa Jiji la Tanga.


Amesema elimu ambayo imekuwa ikitolewa imewajengea uelewa wananchi wa kutambua umuhimu na faida ya kulipa kodi na maendeleo ya Taifa.


"Tangu tulipoanza kutoa elimu kwa mlipakodi miongoni mwa manufaa yaliyopatikana ni pamoja na ukusanyaji wa mapato kuongezeka na wafanyabiashara kutowakinbia maafisa wa TRÀ baada ya kubaini kuwa si maadui"amesema Salim.


Amesema TRA inatambua kuwa utoaji wa elimu kwa walipa kodi ni jukumu endelevu, hivyo itaendelea kuwekeza katika programu mbalimbali za kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu sheria, taratibu na wajibu wao wa kikodi.


“Tunatambua jukumu la elimu ni endelevu. Tumekuwa tukiwekeza kwenye elimu na tutaendelea kufanya hivyo ili wafanyabiashara wapate uelewa wa kutosha na hatimaye kwenda kutekeleza sheria husika kwa wepesi,” amesema Salim


Amesema TRA imekuwa ikitumia njia mbalimbali kutoa elimu, ikiwemo mafunzo ya ana kwa ana, vipindi vya redio pamoja na mitandao ya kijamii.


Kwa mujibu wa Bakar, matumizi ya mitandao ya kijamii yameongezwa kutokana na mabadiliko ya tabia za walipa kodi, ambao sasa wanahitaji kupata taarifa na huduma kwa njia rahisi na za haraka.


Aidha, alisema TRA imeendelea kurahisisha huduma kwa kutumia mifumo ya kidijitali inayowawezesha wafanyabiashara kupata huduma mbalimbali bila kufika moja kwa moja katika ofisi za TRA.


Alisema mamlaka hiyo itaendelea kutangaza huduma hizo na kuwekeza zaidi katika elimu kwa walipa kodi, akisisitiza kuwa uelewa wa sheria za kodi ni miongoni mwa nguzo muhimu za kuongeza utii wa hiari na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.


Wafanyabiashara waliopata nafasi ya kuzungumza katika mafunzo hayo wameomba kuboreshwa zaidi kwa mifumo ya utoaji taarifa kila linapojitokeza tukio jipya.


      MWISHO

No comments: