TAWA, SOAT WAKUTANA KUJADILI MAENDELEO YA UTEKELEZAJI WA SWICA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 13 August 2026

TAWA, SOAT WAKUTANA KUJADILI MAENDELEO YA UTEKELEZAJI WA SWICA

 




Mussa Juma,


maipacarusha20@gmail.com 


Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)  imekutana na wadau wa Chama cha Wawekezaji Mahiri  (SWICA Operators Association of Tanzania – SOAT) jijini Dodoma kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mikataba ya uwekezaji mahiri (SWICA) na kuweka mikakati ya kuongeza tija kwa Serikali, wawekezaji na jamii.


Kikao hicho kilichoongozwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mlage Yussuf Kabange ni sehemu ya juhudi za Mamlaka za kuimarisha ushirikiano na wawekezaji, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kujenga mfumo bora wa mawasiliano kati ya TAWA na kampuni zinazotekeleza shughuli za SWICA na wadau wengine.


Akizungumza katika kikao hicho  August 12 , Kabange amewapongeza wawekezaji hao kwa mchango wanaoutoa katika maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo yao ya uwekezaji ikiwemo kusaidia ujenzi wa madarasa na zahanati, kutoa madawati, kusaidia shughuli za michezo kwa vijana pamoja na miradi mingine ya kijamii.


Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wawekezaji hao katika kuchochea maendeleo ya jamii sambamba na kusaidia juhudi za uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori.


Aidha, Kabange amewahimiza wawekezaji hao kutumia fursa zinazotarajiwa kutokana na mashindano ya AFCON 2027 kwa kuwekeza katika maeneo ya kimkakati yanayosimamiwa na TAWA yakiwemo Makuyuni Wildlife Park mkoani Arusha, Hifadhi ya Pande jijini Dar es Salaam na Hifadhi ya Wami-Mbiki inayopakana na mikoa ya Pwani na Morogoro.


Ameeleza kuwa maeneo hayo yana fursa mbalimbali za uwekezaji katika huduma za utalii, ikiwemo ujenzi wa "tented lodges", kambi za kitalii na miundombinu mingine ya malazi na huduma ambayo inaweza kusaidia kuhudumia wageni watakaotembelea Tanzania wakati wa mashindano hayo.


Katika hatua nyingine, Kabange amewahakikishia wawekezaji hao kuwa TAWA itaendelea kutoa ushirikiano wa kiwango cha juu na kufanya maboresho katika mifumo ya mawasiliano, ikiwemo kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Mamlaka na kampuni moja moja ili changamoto zinazojitokeza ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.


Kikao hicho ni cha kwanza kati ya TAWA na SOAT tangu kuanzishwa kwa chama hicho Machi 28, 2026 na kimetoa nafasi kwa pande hizo kujadili masuala mbalimbali ya kimkakati na kufikia maazimio ya pamoja yanayolenga kuimarisha utekelezaji wa SWICA na kukuza uwekezaji endelevu.


Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya  Mwiba Holdings Ltd iliyowekeza eneo la SWICA pori la akiba la Maswa,Jean-Claude McMenamin akichangia majadiliano katika kikao hicho aliomba maboresho ya utaratibu wa malipo ya marhaba.


“Malipo ya mrabaha (royalties) na tozo nyingine yanahesabiwa kwa kuzingatia makadirio ya mapato badala ya mapato halisi yanayopatikana"


Alishauri TAWA Malipo yote ya mrabaha na tozo zinazohusiana nayo yahesabiwe kwa kuzingatia mapato halisi yaliyopatikana, badala ya mapato yaliyokadiriwa.


Hata hivyo McMenamin alieleza kuridhishwa na ushirikiano ambao wanapewa na TAWA na Serikali Kwa ujumla katika uwekezaji wao katika maeneo ya SWICA  na kueleza sekta ya utalii itaendelea kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi na huduma za kijamii nchini.


Mwisho 


No comments: