Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
MENEJA wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Mashariki, Mhandisi Lorivii Long'idu, amesema ushiriki wa mamlaka hiyo katika Maonesho ya Nane Nane 2026 unalenga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya teknolojia za ujenzi wa gharama nafuu, pamoja na huduma za nishati na maji.
Mhandisi Long'idu amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kutembelea banda la EWURA katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, mkoani Morogoro.
"EWURA imeshiriki Maonesho ya Nane Nane 2026 kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake. Tunawaomba wananchi kutembelea banda letu ili wajifunze, wajionee teknolojia mbalimbali na kupata elimu kuhusu huduma tunazozisimamia," alisema.
Alisema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza maono ya **Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050**, inayolenga kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha juu, ambapo wastani wa kipato cha mwananchi unatarajiwa kufikia dola za Marekani 7,000.
Aidha, alisema EWURA imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata elimu kuhusu matumizi bora ya nishati, huduma za maji na teknolojia mbalimbali zinazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mhandisi Long'idu aliongeza kuwa katika maonesho hayo, EWURA imekuja na teknolojia ya ujenzi wa gharama nafuu inayolenga kupunguza gharama za ujenzi huku ikihakikisha ubora, usalama na uimara wa majengo.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment