KAMATI YA USHAURI WA KISHERIA MKOA WA KILIMANJARO YAINGILIA KATI NA KUOKOA MAISHA YA WATOTO WALIOKUWA WAKIISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 22 August 2026

KAMATI YA USHAURI WA KISHERIA MKOA WA KILIMANJARO YAINGILIA KATI NA KUOKOA MAISHA YA WATOTO WALIOKUWA WAKIISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU

 


 Mwandishi wetu, Kilimanjaro 


maipacarusha20@gmail.com 


Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa wa Kilimanjaro imewaokoa watoto wanne wa familia moja wenye umri kati ya miaka 10 na 11, baada ya kubainika kuwa  walikuwa wakiishi bila uangalizi wa wazazi tangu Februari mwaka huu katika Mtaa wa Relini, Kata ya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi.


Watoto hao walikutwa tarehe 14 Agosti, 2026 wakiishi katika mazingira magumu na kutegemea msaada wa chakula kutoka kwa majirani ambapo  wawili kati yao, wanafunzi wa darasa la tatu, walikuwa wameacha shule.


Aidha Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, wazazi wa watoto hao waliondoka kwenda kufanya shughuli za kilimo Simanjiro, mkoani Manyara, na kuwaacha watoto hao bila uangalizi wa mzazi.


Wakili wa Serikali Mkoa wa Kilimanjaro na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa huo, Bi. Tamari Mndeme, amesema Kamati  hiyo ilibaini kuwa watoto hao walikuwa wakiishi katika mazingira magumu na yasiyo salama.


*“Watoto hawa bado wanahitaji kulelewa na kuelekezwa, lakini wameachwa wanajisimamia wenyewe, wazazi wameacha kutekeleza wajibu na majukumu yao ya msingi kwa watoto jambo ambalo ni kinyume cha sheria”* amesema Bi. Tamari Mndeme.


Nae Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Sajenti Mwajabu Mzee, amesema mtoto hawezi kujisimamia mwenyewe na kwamba wazazi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata malezi na ulinzi unaostahili.


Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Scolastica Swai, ametoa wito kwa wazazi kutekeleza wajibu wao wa malezi na kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na usalama, akisisitiza kuwa jamii haiwezi kuchukua nafasi ya mzazi katika kumlea mtoto wake.


Watoto hao wamechukuliwa na kupelekwa katika eneo salama huku ufuatiliaji wa wazazi wao ukiendelea.

No comments: